Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU
wa Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Bi.Khanifa Karamagi amewataka
wataalamu wa misitu wilayani humo kuhamasisha wananchi kuanzisha vikundi
vya ufugaji nyuki na kuhakikisha vimesajiliwa kisheria ili viweze
kupata misaada kutoka serikalini.
Bi.Kharamagi aliyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya utundikaji mizinga kitaifa ambapo kimkoa ilifanyika wilayani humo.
Alisema
kuwa kuhamasisha uanzishaji wa vikundi vya ufugaji nyuki na kuhakikisha
vimesajiliwa kisheria ni jambo la msingi katika kuvutia wawekezaji na
kuweza kupatiwa misaada kutoka serikalini na taasisi mbalimbali.
Pia
alisema kuwa rasilimali misitu na nyuki vikiendelezwa kwa manufaa ya
kizazi cha sasa na kijacho na kuhamasisha ufugaji nyuki kwa jamii na
utunzaji wa misitu ili kuongeza mazao ya nyuki kama asali, nta na gundi.
Aidha aliwataka wataalamu wa misitu kuhamasisha watu binafsi kuwa
na mizinga ya kisasa ili kupata mavuno bora na mengi yatokanayo na mazao
ya nyuki.
Kwa upande wake Meneja wa misitu Wilayani humo, Bw.Abdin
Mrema alimweleza mkuu huyo kuwa wananchi wengi wilayani humo bado
hawajahamasika kufuga nyuki pamoja na elimu ya ufahamu kutolewa lakini
inaonekana waliopata elimu hii ni wachache,hivyo inabidi juhudi za
uhamasishaji ziongezeke.
Katika maadhimisho hayo zaidi ya vikundi
kumi na moja vilijitokeza na kupatiwa mizinga ya kisasa na zaidi ya
mizinga arobaini ilitundikwa katika msitu wa Msingisi.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni Boresha ufugaji nyuki linda ubora wa mazao yake.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment