Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa
Ponda amekwaa kisiki mahakamani baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es
Salaam kutupilia mbali maombi yake ya marejeo dhidi ya uamuzi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro.
Sheikh Ponda anakabiliwa na kesi ya jinai namba
128 ya mwaka 2013 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, akikabiliwa
na mashtaka ya kufanya uchochezi katika maeneo mbalimbali mjini Morogoro
na kukaidi amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Sheikh Ponda kupitia kwa Wakili wake Juma Nassoro
aliwasilisha maombi ya marejeo Mahakama Kuu, baada ya Mahakama ya Hakimu
Mkazi Morogoro kutupilia mbali maombi yake ya kumfutia shtaka la
kukaidi amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Katika amri hiyo iliyotolewa Mei 9,2013 na Hakimu
Mkazi, Viktoria Nongwa, Ponda aliamriwa kulinda amani na kutokutenda
kosa lolote kwa kipindi cha miezi 12, baada ya kumtia hatiani katika
kesi ya jinai namba 245 ya mwaka 2012,iliyokuwa ikimkabili na wenzake
49.
Ponda kupitia kwa wakili wake aliiomba Mahakama
hiyo imfutie shtaka hilo akidai kuwa, mahakama hiyo haina mamlaka ya
kusikiliza shtaka hilo.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro katika uamuzi
wake uliotolewa, Oktoba Mosi, 2013, Hakimu Mkazi Richard Kabate
anayesikiliza kesi hiyo, alitupilia mbali maombi hayo alisema mahakama
hiyo inayo mamlaka ya kusikiliza shtaka hilo.
Ni uamuzi huo uliomsukuma Sheikh Ponda kupitia kwa
Wakili wake Nassoro, kukimbilia Mahakama Kuu akiiomba ifanye marejeo ya
uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, kinyume cha matarajio yake ya kupata
unafuu, badala yake jana pia alijikuta akiangukia pua katika maombi yake
hayo baada ya Mahakama Kuu kuyatupilia mbali.
Maombi hayo ya marejeo yalitupiliwa mbali jana na
Jaji Augustine Mwarija aliyekuwa akiyasikiliza baada ya kukubaliana na
hoja za pingamizi lililowekwa na mkurugenzi wa mashtaka.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Mwarija alisema baada ya
kusikiliza hoja za pande zote kuhusiana na pingamizi hilo, anakubaliana
na hoja za Wakili wa Serikali Mkuu, Bernard Kongola maombi hayo
yaliwasilishwa mahakamani hapo kinyume na Sheria.
Jaji Mwarija alisema kama Wakili Kongola
alivyosema, kifungu cha 372 (2), kilichotumika katika maombi hayo
kinazuia maombi ya marejeo ya uamuzi au amri iliyotolewa na mahakama za
chini ambao haumalizi kesi ya jinai.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment