Home » » Washangaa mbunge wao kuitwa ‘mzigo’

Washangaa mbunge wao kuitwa ‘mzigo’

Celina KombaniWANANCHI wilayani Ulanga, Morogoro, wamekuja juu kutokana na mbunge wao, Celina Kombani, ambaye pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, kuhusishwa kuwa ni mmoja wa mawaziri mizigo wakati hakutajwa katika orodha ya viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ziara ya hivi karibuni.
Wananchi hao walitoa kauli hiyo juzi wilayani hapa walipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na suala hilo.
Katika ziara hiyo ya CCM ikiongozwa na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana, mawaziri waliotajwa kuwa mizigo ni pamoja na Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika), Naibu wake, Adam Malima, Dk. Shukuru Kawambwa (Elimu), Profesa Jummane Maghembe (Maji).
Akizungumza kwa niaba ya wenzao, Emanuel Mkalimoto, alieleza katika ziara yake wilayani Ulanga iliyofanyika Agosti mwaka jana, Katibu Mkuu huyo wa CCM aliyekuwa ameambatana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, walisifia utendaji kazi wa Waziri Kombani.
Alisema viongozi hao walieleza wazi kati ya mawaziri wachapa kazi katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, Waziri Kombani ni mmojawapo kuwa amekuwa akitekeleza majukumu yake ipasavyo, lakini anashangazwa na yeye kuhusishwa kuwa ni miongoni mwa mawaziri mizigo.
Naye Stanley Mhina, alisema katika ziara hiyo, viongozi hao walimsifu mbunge huyo kuwa ni mmoja wa watekelezaji wa ilani ya chama hicho katika Jimbo la Ulanga Mashariki kwa kuwaletea maendeleo na hivyo kupunguza kasi ya wapinzani kulinyemelea jimbo hilo.
“ Binafsi nilikuwepo katika ziara nzima ya viongozi wetu wa juu wa CCM, walikuwa wakisifu utendaji wa Waziri Kombani kuanzia wizarani na katika jimbo letu kuwa ni mfano wa kuigwa baada ya kuona maendeleo sasa tunashangazwa leo, je, wamesahau kauli zao?” alihoji Mhina.
Alipotafutwa kutoa ufafanuzi huo, Waziri Kombani alikataa kulizungumzia suala hilo kwa madai sasa lipo katika mamlaka nyingine.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa