MKUU wa Wilaya (DC) ya Mvomero, Anthony Mtaka, mmiliki wa Kiwanda
cha Sukari Mtibwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), wanadaiwa kuukacha
mkutano wa wakulima wa miwa wa nje wa Mtibwa ulioitishwa kujadili
hatima ya deni la sh bilioni 1.9 linalodaiwa na wakulima hao kiwandani
hapo msimu uliopita.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mwishoni mwa wiki kwenye mkutano huo
ulioitishwa na vyama vya siasa kikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
wilayani humo, wakulima hao walisema walisikitishwa na kitendo cha mkuu
huyo wa wilaya kutotokea kwenye mkutano huo.
“Sisi ni wanyonge hatuwezi kuwafanya kitu…unadhani hata wakija hapa
watasema nini kama wamechukua miwa yetu tangu Agosti 2013 na
hawajatulipa? Dawa ni kuvamia kiwanda tugawane kilichopo,” alisema
Julius Shekilima wa Kidudwe.
Walisema mkuu huyo wa wilaya amekuwa hana msaada kwao, kwani licha
ya kumfikishia tatizo la kutolipwa fedha zao kwa zaidi ya mara tano
aliahidi kufuatilia bila mafanikio.
“Sasa watoto hawasomi, hatuna fedha za kujikimu, tumekopa kila kona
hadi hatutoki majumbani, tukiuuliza uongozi wa kiwanda hauna jibu zaidi
ya kutukejeli na kutudharau eti madai yetu hayakitishi kiwanda,”
alisema Husina Saleh wa Madizini.
Waandaaji wa mkutano huo akiwemo Diwani wa Mtibwa, Lucas Mwakambaya,
walifafanua kuwa uwepo wa mkutano huo haukuwa siri kwani wakulima,
mmiliki wa kiwanda na mkuu huyo wa wilaya walikuwa na taarifa isipokuwa
walipuuza.
“Unajua hizi kazi za kuwatumikia wananchi zinahitaji wenye nia
thabiti ya kuwatumikia wananchi. Mfano hili suala ukilianagalia kwa
mfumo wa serikali tuliyonayo ni hadi yatokee maafa utaona msururu wa
viongozi hata wasiotarajiwa kufika huku daima,” alifafanua Mwaka Mbaya.
Alieleza inashangaza wanachi waliosota mwaka mzima hawalipwi madai
yao halali na hakuna hata jibu kwa umma juu ya ucheleweshwaji.
Kutokana na hali hiyo, wakulima hao walikubaliana kesho kuingia
kiwandani hapo kwa nguvu kushinikiza walipwe fedha zao vinginevyo aende
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutatua mgogoro huo.
“Ndugu zetu si wakulima wanaodai kiwanda hiki, wastaafu wa mwaka jana
walilipwa kiwango cha makadirio ya shilingi 700,000 kati ya shilingi
milioni tano hadi 10, eti fedha nyingine watalipwa kwa awamu,”
aliongeza.
Mtaka alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi juu ya kutotokea kwenye
mkutano huo, alijibu kwa ukali na kwa kifupi, akimtaka mwandishi
kuandika ajuavyo.
“Sina sababu yoyote ya kutohudhuria mkutano ule…wewe andika ujuavyo bwana…” alisema Mtaka kisha kukata simu.
Kiwanda cha Sukari Mtibwa wilayani Mvomero kimekuwa na mgogoro na wakulima na wafanyakazi wake kwa muda mrefu sasa.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment