Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Kamati hiyo hiyo ilianza kufanya kazi Desemba mwaka jana kwa kutembelea vituo mbalimbali vya mizani mikoani ili kubaini sababu zilizosababisha kuwapo kwa mgogoro baina ya Serikali na wadau wa usafirishaji.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florence Turuka, aliliambia NIPASHE kuwa timu hiyo imesharejea kutoka mikoani na kukabidhi ripoti kwake.
Dk. Turuka alisema baada ya timu hiyo kukabidhi ripoti hiyo, hatua inayoifuata ni kuipitia na baadaye ataikabidhi kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Bila kueleza lini ripoti hiyo itatolewa majibu, Dk. Turuka alisema Waziri Mkuu ndiye atakayetoa majibu ya ripoti hiyo baada ya kukabidhiwa na kuipitia.
“Kimsingi, ile timu imeshamaliza kazi yake na wamenikabidhi ripoti, hatua inayofuata sasa ni mimi kuipitia na kumkabidhi Waziri Mkuu ambaye yeye ndiye atakayetoa majibu,” alisema Dk. Turuka.
Novemba 24, mwaka jana, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema ataisimamia sheria namba 30 ya mwaka 1973 ya usalama barabarani iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2001 inayohusu kiwango cha mwisho cha uzito wa magari pasipo kumwogopa mtu yeyote kwa kuyatoza magari yote yatakayozidisha uzito.
Dk. Magufuli alitolea mfano wa viwango vya uzito kwa magari ya mizigo katika nchi nyingine kwa Marekani ni tani 36.2, Uingereza tani 40, Ujerumani tani 40, Ufarasa tani 40, Urusi tani 38, lakini kwa Tanzania ni tani 56 ambacho ni kiwango kikubwa.
Chama cha Wamiliki wa Malori (Tatoa) na Chama cha wamiliki wa Mabasi (Taboa) waliingia katika mgogoro na serikali baada ya kupinga tangazo lililotolewa na Serikali Oktoba Mosi, mwaka jana kubatilisha msamaha wa kutotoza faini magari yanayozidisha uzito kwa asilimia tano.
Tatoa na Taboa Oktoba 8 na 9, mwaka jana waligoma wakipinga kufutiwa msahama wa kutozwa faini asilimia tano kwa kuzidisha uzito kupitia tangazo la Serikali lililotolewa na Waziri Magufuli na kurejesha sheria ya mwaka 1973.
Baada ya mgomo huo uliotikisa nchi, Oktoba 10, Pinda aliingilia kati na kusitisha tangazo la Dk. Magufuli huku akitoa mwezi mmoja kwa serikali kukutana na wadau wa usafirishaji kupata mwafaka.
Mbali na Tatoa na Taboa, kamati hiyo pia iliwahusisha wajumbe kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, Viwanda na Biashara, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mgomo wa wasafirishaji ulisababisha Bandari ya Dar es Salaam kuelemewa mizigo.
Takribani tani 23,165 za mbolea ambayo ilikuwa imeshushwa bandarini hapo ilikwama kutokana na kutokuwapo kwa malori. Kadhalika, meli tisa za mizigo zilikwama kushusha na kupakia mizigo bandarini na kushuka kupungua kwa uwezo wa kushusha makontena.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment