Kinyume na matarajio ya wengi, mradi wa Upanuzi wa Barabara ya
Morogoro, kilomita 21 kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi
Kimara umekuwa kero kubwa kwa wananchi wanaotumia vyombo vya usafiri
kupitia katika barabara hiyo. Tangu kuanza kwa mradi huo yapata miaka
miwili hivi iliyopita, tumeshuhudia wananchi wengi wanaotumia barabara
hiyo wakionyesha kuchoshwa na adha wanazozipata kutokana na misururu
mirefu ya magari barabarani.
Madereva na abiria wanaotumia barabara hiyo na
nyingine nyingi zinazokatiza kutoka sehemu mbalimbali za jiji sasa
wanauona upanuzi wa barabara hiyo kama laana badala ya faraja. Wapo
wanaosema mradi huo ni wa ovyo. Mbunge mmoja alisema bungeni mjini
Dodoma hivi karibuni kwamba misururu ya magari ambayo kwa kiasi kikubwa
inasababishwa na mradi huo ni janga la kitaifa.
Kauli za aina hiyo ni kielelezo tosha kwamba
watumiaji wa barabara hiyo wamechoshwa na adha zinazosababishwa na
upanuzi wa barabara hiyo, ambao unaonekana kutokuwa na mwelekeo na
usimamizi makini. Siyo jambo la kufikirika hata kidogo kwamba inachukua
zaidi ya saa tatu au nne kutoka katikati ya Jiji hadi Kimara au kutoka
Tazara hadi Mwenge au kutoka makutano ya Barabara za Nyerere na Kawawa
hadi Kawe kupitia Magomeni. Umuhimu wa Barabara ya Morogoro kwa wasafiri
na vyombo vya usafiri ni mkubwa mno kwa sababu ni kiunganishi kikubwa
cha barabara nyingi, zikiwamo za Ali Hassan Mwinyi na Kilwa zinazoingia
na kutoka jijini kama ilivyo Barabara ya Morogoro.
Zipo taarifa nyingi zinazoeleza jinsi kadhia ya
msongamano wa magari jijini ulivyosababisha migogoro ya kifamilia na
katika sehemu za kazi. Kuchelewa sana kufika nyumbani kutoka kazini
kumeelezwa kusababisha ugomvi wa mume na mke kwa kutuhumiana kukosa
uaminifu, kama ilivyo kwa wafanyakazi wanaotuhumiwa na waajiri wao kwa
uzembe na hujuma kutokana na kuchelewa kazini kwa ‘kisingizio cha foleni
barabarani’.
Pamoja na athari hizo za kijamii, zipo athari
kubwa za kiuchumi. Msongamano wa magari baada ya kuanza mradi huo wa
Barabara ya Morogoro unakadiriwa kuwa zaidi ya Sh4 bilioni kila siku
zikiwa ni gharama za petroli na dizeli, mbali na wafanyakazi na
wafanyabiashara kupoteza muda mrefu (man hours) njiani kabla ya kufika
katika sehemu zao za kazi.
Lakini nani anajali? Inaonekana kwamba TANROADS
inayopaswa kuisimamia Kampuni ya Strabag inayopanua barabara hiyo
imeshindwa kufanya hivyo. Matokeo yake ni kwamba kampuni hiyo inafanya
itakavyo kwa kufunga michepuo ya barabara zinazoingia au kutoka katika
Barabara ya Morogoro pasipo kutoa taarifa wala kuonyesha alama zozote.
Hicho ndicho chanzo cha vurugu na sintofahamu kubwa, kwani magari
yanashindwa kwenda mbele ama kurudi nyuma, hivyo kusababisha msongamano
mkubwa barabarani.
Maswali bado yanaulizwa kama kweli mradi huo
ukikamilika utaweza kupunguza msongamano wa magari jijini, kwani
tathmini nyingi zimeonyesha kwamba ni barabara za juu (fly-overs) na
usafiri wa reli ndiyo pekee unaoweza kupunguza au kumaliza msongamano wa
magari barabarani. Tunaitaka Serikali, kupitia TANROADS iisimamie
Kampuni ya Strabag isifanye kazi yake kihuni kama inavyofanya hivi sasa.
Ikumbukwe kwamba Jiji la Dar es Salaam ndiyo mhimili mkubwa wa uchumi
wa nchi yetu. Kinachofanywa na Strabag ni sawa na kuhujumu uchumi wetu.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment