Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akikagua Daraja la Mto Mkundi mkoani
Morogoro linalokarabatiwa baada ya kuharibiwa na mafuriko hivi
karibuni.Rais Kikwete alitembelea eneo hilo na sehemu nyingine
zilizokumbwa na mafuriko hayo kujionea uharibifu. (Picha na Freddy Maro
wa Ikulu)
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi
na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameliamuru Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanza mara moja kazi ya kusimamia utoaji
huduma kwa watu walioathiriwa na mafuriko katika Mkoa wa Morogoro, ikiwa
ni pamoja na kusimamia ujenzi wa nyumba za muda kwa wahanga hao.
Rais pia
ameliamuru Jeshi kupeleka mashine za kusafisha maji katika makambi
ambako wahanga hao wa mafuriko ya Januari 22, mwaka huu wanaishi kwa
muda.
Aidha, Rais
Kikwete amewahakikishia wahanga wa mafuriko hayo kuwa Serikali
itahakikisha inawapatia huduma zote za msingi ikiwa ni pamoja na
chakula, malazi, maji na huduma za afya hadi hapo watakapokuwa na uwezo
wa kuanza kujitegemea tena.
Rais
Kikwete ametoa amri hizo kwa Jeshi jana, Januari 27, 2014, wakati
alipotembelea kambi za wahanga wa mafuriko hayo kuwajulia hali
walioathirika katika makambi yaliyoko Shule ya Sekondari ya Magole
katika eneo la Dumila na katika Kijiji cha Mateteni kilichoko Dakawa,
Wilaya ya Kilosa.
Katika
hotuba zake fupi baada ya kuwa ametembelea na kuona mahema ambamo
wahanga hao wanalala, Rais Kikwete amesema ameagiza Jeshi kuongoza
harakati za kuwahudumia wahanga hao kwa sababu zikifuatwa taratibu za
kawaida za Kiserikali huduma zitachelewa sana kuwafikia waathirika.
“Kazi
yetu ni kusimamia maisha ya watu hasa kipindi cha shida za namna hii.
Tukifuata taratibu za kawaida za Kiserikali za tenda tutachelewesha sana
huduma za dharura kwa waathirika. Ndiyo maana nimeliamuru Jeshi kufanya
kazi hii ikiwa ni pamoja na kujenga haraka makazi ya muda kwa
waathirika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika
mazungumzo hayo na Mkuu wa Majeshi, nimemwagiza pia kuleta mashine za
kusafishia maji ili kuhakikisha kuwa watu wanakunywa maji salama kwa
sababu katika hali ya sasa maji yasiyokuwa salama yanaweza kuwa chanzo
cha magonjwa.”
Kuhusu
upatikanaji wa chakula cha msaada kwa wahanga, Rais Kikwete amesema kuwa
Serikali inacho chakula cha kutosha kwa ajili yao. “Tunacho
chakula cha kutosha na hata kile tusichokuwa nacho tutanunua. Tutabanana
ndani ya Serikali ili tupate fedha za kutosha za kuwahudumia.”
Kuhusu malazi, Rais amesema:”Naambiwa
kuna upungufu wa magodoro. Tutahakikisha kuwa yanapatikana na yatafika
katika siku mbili zijazo. Hatutaki watu walale chini na waje kupata
vichomi.”
Kuhusu maji, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa huduma ya maji bure kwa wahanga. “Tutaendelea kutoa bure huduma hii mpaka hapo huduma ya kawaida ya maji itakapoanza kupatikana tena.”
Kuhusu
huduma za afya, Rais amesema kuwa anafurahi kuwa kila kambi ya wahanga
inayo huduma ya afya ambayo itaendelea kutolewa kwa kadri watu
wanavyozidi kuishi kwenye makambi.
Rais
ameagiza kuwa baada ya muda mfupi viongozi wa Mkoa wa Morogoro na wilaya
husika wakae chini na viongozi wa ngazi za chini na wahanga kujadili na
kutafuta mwafaka kuhusu maisha ya baadaye ya wahanga – hasa kuhusu
namna gani wanaweza kupatiwa maeneo yaliyoko nje ya mikondo ya mafuriko.
“Hili
ni lazima kwa sababu hata kama imechukua miaka mingi kwa mafuriko ya
sasa kutokea ni dhahiri kuwa iko siku yatakuja tena – inaweza kuwa hata
mwaka huu kwa sababu zipo mvua za masika. Kwa hiyo ni lazima tukubaliane
jinsi gani ya kurudi ama kutokurudi katika maeneo yetu tulikotoka.”
0 comments:
Post a Comment