Home » » Usalama Mvomero haujaimarika

Usalama Mvomero haujaimarika

Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Morogoro, John Laswai
Hali ya usalama haijawa shwari katika Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro kati ya wakulima na wafugaji baada ya kundi la vijana wafugaji kuvamia gari walilopanda wakulima na kuwapa vipigo na kuwajeruhi.

Katika tukio hilo, mfugaji mmoja alifariki dunia baada ya kugongwa na gari lililokuwa limewabeba wakulima waliokuwa wakitoka kuandaa mashamba eneo la Mgongola.
Tukio hilo limetokea juzi wakati wakulima hao wakiwa ndani ya gari  aina ya Isuzu baada ya kufika eneo la Kambala na ghafla kusimamishwa na kundi la  morani wa Kimasai.

Mmoja wa wakulima hao, Omar Hamad, alisema wakiwa ndani ya gari hilo yeye na wenzake watano walisimamishwa, lakini dereva wao alitakaa na alipoendelea mbele alikuta magogo yamepangwa barabarani na kulazimika kusimama.

Alisema ghafla kikundi cha morani kiliwavamia na kuanza kuwashambulia kwa kutumia silaha mbalimbali na baadhi yao kujeruhiwa na kuamua kukimbilia porini kuokoa maisha yao.

Alisema baada  kuona mashambulizi yanaongezeka, dereva aliamua kulitoa gari hilo kwa kasi na ndipo mbele yake alikutana na pikipiki iliyokuwa inakuja mbele yao , lakini ilipoteza mwelekeo na gari kuigonga na kusababisha kifo cha dereva wa pikipiki hiyo ambaye alikuwa mfugaji.

Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Morogoro, John Laswai, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea jioni katika kijiji cha Kambala.
Alisema tayari Jeshi la Polisi limetuma askari katika eneo hilo kwa ajili ya kuwasaka morani hao.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa