Wiki iliyopita nilikwenda Morogoro ambako pamoja na mambo
mengine nilikuwa na kipindi kwenye televisheni moja mkoani humo,
kilicholenga kutoa ushauri kwa jamii kuhusu namna ya kupambana na
changamoto za maisha. Baadaye nilikutana na watu waliokuja kwenye hoteli
niliyokuwepo kwa lengo la kubadilishana mawazo zaidi kuhusiana na yale
ambayo niliyaeleza kwenye televisheni. Mmoja wa watu alikuwa ni Erick
Mtengele, kijana wa Kimasai ambaye amekuwa akihangaika huku na kule
kutafuta namna ya kuwasaidia wafugaji nchini.
“Mimi ni kati ya Wamasai wachache nchini walio na
elimu ya chuo kikuu, nimehitimu elimu ya maendeleo ya jamii katika Chuo
Kikuu cha Tumaini mwaka 2010, kwa bahati mbaya hadi leo sina ajira,”
anasema Mtengele ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Luganga, Kata ya Ilala
Mpya, mkoani Iringa.
Tulizungumza mengi, yakiwemo matatizo ya sekta ya
elimu nchini na harakati zake za kuwasaidia wanafunzi wa Shule ya
Sekondari ya William Lukuvi wapate angalau bweni, akisema kuwa ameandika
barua maeneo kadhaa kuomba shule hiyo ijengewe bweni bila mafanikio.
“Shule haina mabweni, wanafunzi wanalala kwenye madarasa,” anasema Mtengele.
Baada ya mazungumzo hayo nililazimika kufuatilia
ili kujua ukweli, nilibaini kuwa ni ukweli thabiti kwamba wapo wanafunzi
wanalala kwenye madarasa katika shule hiyo, sababu kubwa ni kwamba
shule haina uwezo wa kifedha wa kujenga mabweni.
“Huogopi kufuatilia shule hii?” anaonya mwandishi
mmoja wa habari anayefanyia kazi mkoani Iringa kwa maelezo kuwa
kufuatilia shule hiyo kunaweza kuzusha kutokuelewana na baadhi ya watu
ambao kwa namna moja ama nyingine wanahusika na shule hiyo.
Mwandishi huyo anaonya kuwa hofu ya kufanyiwa
mabaya ndiyo sababu waandishi walio wengi wanaogopa kuandika ukweli
kuhusiana na shule hiyo kwamba baadhi ya wanafunzi wanalala katika
madarasa tofauti katika shule hiyo.
“Kuna waandishi waliwahi kufuatilia suala hili na
kuhoji kwa nini mabweni hayajengwi, matokeo yake siyo tu kwamba
hawakupewa ushirikiano na wale ambao wanahusika kutolea maelezo jambo
hilo, bali walionekana kama wanaingilia mambo yasiyowahusu, wengine hata
wakajikuta katika hofu kuhusu maisha yao,” alionya mwandishi huyo.
Hata hivyo niliendelea kufuatilia kutokana na
ukweli kwamba lengo la makala hii siyo kudhalilisha yeyote, bali kueleza
ukweli ili kuangalia namna gani wanafunzi wanaweza kusaidiwa kwa
kujengewa mabweni.
Kama yupo mwenye nguvu za kusumbua wale ambao
wanaeleza ukweli kuhusiana na hali mbaya ya maisha ya wanafunzi kwa
kukosa mabweni, nguvu hizo azielekeze kuhakikisha mabweni yanajengwa,
tena ikiwezekana haraka.
Nguvu zake zitakuwa za maana zaidi ikiwa
atafikiria namna ya kusaidia kupatikana kwa mabweni kuliko kukasirika
kwa sababu ya kuandikwa ukweli kwamba Shule ya Sekondari William Lukuvi
haina mabweni kiasi kwamba wanafunzi wanalazimika kulala darasani.
Katika kufuatilia ilibainika kuwa ni kweli kuna
ugumu wa kupata ushirikiano, na pia hata baadhi ya waandishi wa habari
wana hofu, kwa mfano kuna mwandishi alifanikiwa kupiga picha miezi
kadhaa iliyopita wanafunzi wakiwa darasani wamelala, hakuweza kuzitumia,
huku ulinzi ukiwekwa kuhakikisha hakuna mwandishi anayefanikiwa
kufahamu hali hiyo ya watoto kulala darasani.
chanzo;mwananchi
chanzo;mwananchi
0 comments:
Post a Comment