HALMASHAURI ya Manispaa ya Morogoro inatarajia
kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa mkoani hapa kwa
kujenga hospitali ya wilaya ya manispaa hiyo katika eneo la Kikundi, nje kidogo
ya mji kwa gharama ya sh bilioni mbili.
Meya wa Manispaa ya Morogoro, Amir Nondo,
alibainisha hayo mjini hapa jana alipozungumza na waandishi wa habari na kusema
kuwa tayari mkataba wa ujenzi huo umesainiwa na Kampuni ya Mzinga Co-operation
kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Nondo alisema kampuni hiyo itaanza na ujenzi wa
nyumba ya mapokezi ambayo itakamilika katika kipindi cha siku tisini na kwa
gharama ya sh milioni 548 na baadaye kuendelea na majengo mengine.
Alisema ujenzi wa hospitali hiyo utasaidia
kupunguza msongamano kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa ambapo mgonjwa atatibiwa
kwenye zahanati za kata na ikishindikana atapelekwa kwenye hospitali hiyo.
“Lengo letu mgonjwa ikishindikana kutibiwa kwenye
zahanati zetu ambazo tumejenga kila kata, atapewa rufaa kwenda hospitali ya wilaya
na hapo kama bado atapelekwa hospitali ya rufaa ya mkoa, si mtu anapata kihoma
kidogo anakimbilia hospitali ya mkoa, tunataka kupunguza mrundikano wa
wagonjwa,” alisema.
Pia alibainisha hospitali hiyo inatarajia kujengwa
katika kipindi cha mwaka mmoja, na kwamba hadi kufikia mwaka 2014 mwishoni
wanatarajia huduma iwe imeanza kutolewa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment