Home » » Bendera: Nitazifanyia kazi changamoto zao la tumbaku

Bendera: Nitazifanyia kazi changamoto zao la tumbaku

SEKTA ndogo ya tumbaku nchini inakabiliwa na changamoto kadhaa na endapo zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu, zao hilo litawanufaisha maradufu Watanzania.
Mkurugenzi wa mambo ya sheria wa kampuni za Tanzania Leaf Tobacco (TLTC) pamoja na Tanzania Tobacco Processors Limited (TTPL), Richard Sinamtwa, aliorodhesha changamoto kadhaa zinazoikabili sekta ndogo ya tumbaku wakati akiwasilisha taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, alipotembelea TTPL.
Alisema sekta hiyo inaandamwa na changamoto nyingi ikiwemo ya tozo, ushuru wa mazao unaolipwa kwa halmashauri za wilaya wakati wa kuvuna tumbaku, ushuru wa huduma ambao unalipwa mahali ambako kiwanda cha kuchakata tumbaku kimejengwa pamoja na kodi inayotokana na faida.
“Hili ni zao lile lile linalotoka shambani hadi kiwandani, lakini linakatwa kodi zaidi ya moja kinyume cha sheria za kodi,” alisema.
Sinamtwa alisema changamoto nyingine inayoikabili sekta ndogo ya tumbaku ni zao hilo kushindwa kupigiwa debe, ili liingie kwenye soko la Marekani kupitia mpango wa ukuzaji fursa za kiuchumi Afrika (Agoa), hasa kwa vile nchi hiyo hutoza ushuru wa idadi maalumu iliyowekwa (TRQ) kwa baadhi ya mazao ya kilimo kama vile cocoa, karanga, sukari na tumbaku.
“Utaratibu wa TRQ unaruhusu idadi maalumu ya bidhaa kuingizwa katika soko la Marekani bila kulipiwa ushuru au kwa kiwango maalumu kwa kipindi fulani cha muda, lakini pale kiwango cha bidhaa kinapozidi idadi inayotakiwa, basi kinakatwa kodi zaidi,” alisema Sinamtwa.
Alimtaka mkuu wa mkoa kufikisha kilio hicho kwa Wizara ya Viwanda na Biashara, ili kuliwezesha zao la tumbaku kuingia kwenye soko la Agoa.
Alisema matatizo mengine yanayokumba uzalishaji wa zao la tumbaku ni uwezo mdogo wa bandari ya Dar es Salaam, ambao unasababisha baadhi ya bidhaa zinazoonekana zinaweza kuharibika haraka pamoja na mafuta kupewa kipaumbele zaidi dhidi ya makontena ya tumbaku na bidhaa nyingine.
“Hali hii inasababisha ucheleweshaji usio wa lazima katika kusafirisha tumbaku, hivyo kuleta athari katika taratibu nzima za kusafirisha tumbaku nje,” aliongeza.
Sinamtwa alisema matatizo mengine yanayoikabili TPPL, ni umeme usioaminika katika uzalishaji, na hivyo kukifanya kiwanda muda mwingi kutumia jenereta.
Kuhusu mafanikio, Sinamtwa alisema ni ongezeko la thamani ya mtaji, ikiwa ni pamoja na mali za kampuni, ambazo zimepanda kutoka dola milioni 15.6 za Marekani mwaka 1997 wakati kampuni iliponunua kiwanda kutoka kwa kampuni iliyokufa ya Tanzania Tobacco Authority hadi kufikia dola milioni 57 mwaka 2012, ongezeko ambalo ni takriban asilimia 276.
Pia kodi inayokatwa baada ya faida ilipanda kutoka sh bilioni 1.7 mwaka 2008 hadi sh bilioni 2.2 mwaka jana huku gawio wanalopata wadau likipanda kutoka sh milioni 104 mwaka 2008 hadi sh milioni 165 mwaka jana.
Mkuu wa Mkoa, Bendera, aliahidi kufanyia kazi changamoto zinazokabili uzalishaji wa tumbaku nchini kwa kuwasiliana na mamlaka zinazohusika.
Akitoa neno la shukrani, mkurugenzi mkuu wa makampuni hayo mawili, Paul Crossan, alimshukuru Bendera kwa kuwatembelea, akisema ni ziara aliyoifanya kwa wakati muafaka na ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya sekta ndogo ya tumbaku.
Chanzo: Tanzania Daima


0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa