ZAIDI ya asilimia 80 ya watumishi wa Jumuiya ya
Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamefukuzwa kazi kwa tuhuma za kusababisha
madeni na miradi ikiwamo shule kufilisika.
Mjumbe wa Baraza Kuu la jumuiya hiyo taifa, William
Malecela, alisema hayo wakati wa mkutano wa ndani wa Halmashauri Kuu ya CCM
Manispaa ya Morogoro na kudai kuwa watumishi wengine zaidi watafukuzwa
ili kuiweka jumuiya hiyo katika hali nzuri na kurudi katika heshima yake.
“Watumishi wengi wameiingiza jumuiya katika madeni
makubwa na kuiacha haina fedha na hata miradi yetu mbalimbali ya
maendeleo kama shule inakufa sasa, tunataka turudi katika msitari,” alisema
Malecela.
Alisema uongozi wa sasa umekusudia kuifufua upya
jumuiya hiyo, na wale wanaoona hawawezi kwenda na kasi iliyopo, ni vema wakajiondoa
wenyewe na kupisha wengine.
“Tuliingia madarakani akaunti ya jumuiya ikiwa
haina senti, lakini sasa akaunti ina fedha, hata mikutano ya baraza
tunaiendesha kwa kujilipa wenyewe, hatutegemei kuomba.
“Mwakani kama mambo yatakwenda vizuri, tumekusudia
kila mkoa kuwa na gari, wilaya kuwa na pikipiki na kata baiskeli, ingawa wapo
wasiotutakia mema kutokana na kuwanyima ugali kutokana na namna walivyokuwa
wameigeuza jumuiya hii,” alisema Malecela.
Akiwa Morogoro Vijijini, Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazazi, Abdallah Bulembo, aliwaasa madiwani kutogeuka miungu watu katika maeneo
yao, na kuwataka kuthamini chama kilichowatuma katika nafasi hizo, badala ya
kujiona wao ni watumishi wa serikali.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment