UMOJA wa Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), umesema haupo tayari kuona unaingiliwa na wanasiasa kwa ajili ya kutaka waungwe mkono kuelekea katika uchaguzi mkuu wa urais wa mwaka 2015.
Tahadhari hiyo imetolewa na Mwenyekiti mpya wa Umoja huo, Francisco John wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii baada ya kuchaguliwa kushika wadhifa huo katika mkutano mkuu, uliofanyika mjini hapa juzi.
Wajumbe kutoka vya vyuo 35, 44 wa Tahliso nchini walishiriki kwenye uchaguzi huo. “Tutasimama kutetea mambo ya msingi wanayotutuma wanachama wetu , wanasiasa wakae mbali nasi, kamwe wasitarajie tutavutika nao kuelekea uchaguzi mkuu ujao... tunawaomba waiache mbali Tahliso ifanye shughuli zake za wanafunzi,“ alisema John.
Alisema kimsingi Tahliso ni taasisi isiyo ya kiserikali isiyofungamana na upande wowote na majukumu yake yameainishwa kwenye katiba, iliyoanzisha umoja huo.
Mwenyekiti huyo alisema Tahliso ni chombo kinachowaunganisha wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini, kujadili masuala ya elimu na kuyawasilisha sehemu husika ili yapatiwe ufumbuzi na wahusika wakuu.
Aliahidi viongozi wapya watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa yaliyomo kwenye katiba ya Tahliso na si kwenda kinyume, kutokana na msukumo wa baadhi ya wanasiasa wenye malengo ya uchaguzi mkuu ujao.
Mwenyekiti huyo alielezea kuwa ataitisha mkutano mkuu wajumbe kutoka vyuo vyote vya elimu ya juu nchini ili kurejea upya maudhui ya Tahliso kwa lengo la kuondoa migongano inayojitokeza kila mara.
Chanzo:Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment