Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
JUMUIYA ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani
Mvomero, Morogoro, imeingia kwenye malumbano na Baraza la Madiwani
baada ya mwenyekiti wa jumuiya hiyo kuwaita madiwani ‘mizigo, wazee,
viwete na hawana tija’ ndani ya chama.
Hali hiyo ilijitokeza baada ya Mwenyekiti wa umoja huo, Paschal Boga,
katika kikao cha Baraza la Vijana wa chama hicho kilichoketi Februari
15, mwaka huu kuwatuhumu madiwani wa halmashauri hiyo kuwa ni mzigo
kwenye chama kwa kushindwa kutekeleza ilani ya chama na kutetea maslahi
ya wananchi.
Mmoja wa wajumbe kwenye kikao hicho ambaye hakutaka jina litajwe,
alisema malumbano hayo yaliyosababisha wajumbe hao kurushiana maneno
makali na vitisho, yalianza baada ya baadhi ya wajumbe kuhoji zilizopo
fedha asilimia tano ya pato la halmashauri zinazotakiwa kupelekwa kwa
makundi ya vijana na wanawake.
Alisema baada ya kuibuliwa kwa hoja hiyo na kumlazimu ofisa utamaduni
wa halmashauri hiyo kusema fedha zimekuwa zikitolewa tangu mwaka 2009
bila takwimu, wajumbe walipinga wakimtaka alete takwimu hizo kwa kuwa
kundi hilo limetelekezwa kwa kukosa fursa ya uwezeshwaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jonas Zeeland,
alisema hali hiyo ipo ila tayari madiwani wameamua kumwandikia barua
katibu wa CCM wilaya ili amshugulikie ofisa huyo.
“Sisi Baraza la Madiwani tumekubaliana kumpa siku 14 athibitishe
kwetu na ndani ya chama kauli yake hiyo ya kibaguzi ikiwemo uzembe wetu
vikaoni,” alisema Zeeland.
Alisema madiwani wamesikitishwa na kauli hiyo inayowakatisha tamaa
ikilinganishwa takribani mwezi mmoja uliopita CCM ikiwakilishwa na
wenyekiti wote akiwemo Boga, ilitoa hati kwa madiwani kushukuru dhidi
ya utumishi bora ndani ya halmashauri.
Zeeland aliongeza kuwa halmashauri imejipanga kuhakikisha wanapata
hati safi kwa mara ya kwanza toka ianzishwe 2003 na hiyo inatokana na
kazi iliyofanywa na madiwani waliojitoa muhanga kwa kuisafisha
halmashauri, ikiwemo kuwaondoa na kuwashitaki watendaji waliokuwa
kikwazo cha maendeleo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment