Home » » Baraza la wafanyakazi Siri ya utendaji bora

Baraza la wafanyakazi Siri ya utendaji bora

Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Wafanyakazi la Sita la TMDA limefanyika kwa ufanisi tarehe 5-6 Februari, 2026 katika Manispaa ya Morogoro, kwa kuwakutanisha wajumbe wa Menejimenti na kutoka kwa Watumishi wa TMDA kwa lengo la kujadili na kukubaliana masuala mbalimbali ya kitaasisi yenye mchango mkubwa katika kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka.

Miongoni mwa ajenda kuu zilizojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na kutoa maoni na mapendekezo kuhusu Mpango Mkakati wa TMDA wa miaka mitano (2026/27 – 2030/31), Rasimu ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2026/27, pamoja na Mpango wa Mazingira, Jamii na Utawala (Environmental, Social and Governance – ESG).

Akifunga kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Dkt. Adam Fimbo, aliwashukuru wajumbe wa Baraza kwa maoni yao ambayo yalilenga kujenga na yanayolenga kuboresha utendaji kazi wa taasisi, akisisitiza kuwa wafanyakazi ni sehemu muhimu ya TMDA na mchango wao ni nguzo ya mafanikio ya Mamlaka.

“Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu la ushirikishwaji na uwazi katika maamuzi ya taasisi. Mawazo na maoni yenu yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mifumo ya utendaji na kulinda afya ya jamii,” alisema Dkt. Fimbo.

Baraza la Wafanyakazi la TMDA linajumuisha wawakilishi kutoka Menejimenti na Watumishi, na hukutana mara mbili kwa mwaka kwa mujibu wa sheria na miongozo ya utumishi wa umma.

Lengo kuu la mikutano hiyo ni kujadili taarifa za utendaji kazi wa TMDA, kubaini fursa na changamoto zilizopo, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha mifumo na huduma za Mamlaka.

Kupitia Baraza la Wafanyakazi, TMDA imekuwa ikiimarisha mshikamano, uwajibikaji na mawasiliano ya wazi kati ya Menejimenti na Watumishi, hali inayosaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na bidhaa zingine zinazodhibitiwa, kwa lengo la kulinda afya ya jamii.

TMDA itaendelea kuthamini mchango wa Baraza la Wafanyakazi kama chombo muhimu cha ushirikishwaji katika maamuzi ya kimkakati na uendeshaji wa taasisi, sambamba na azma ya kujenga mazingira bora ya kazi na kutoa huduma bora kwa jamii.


0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa