Imeandikwa na Mwandishi Wetu
TANZANIA kuanzia Januari mwakani itarejea kwa kishindo katika soko la
nyama la kimataifa wakati kiwanda cha nyama cha kisasa cha machinjio na
usindikaji cha Nguru Hills kilichopo Mvomero, Morogoro kitakapoanza
kazi.
Kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 300 na mbuzi
2,000 kwa siku. Ujio wa kiwanda cha Nguru unaleta matumaini mapya kwa
sekta ya nyama baada ya Tanzania kutamba kati ya mwaka 1947 na 1975
kupitia kiwanda cha Tanganyika Packers Ltd (TPL) ambacho kilisafirisha
nyama iliyosindikwa hadi soko la Ulaya.
Wakati huo kiwanda hicho kilipokuwa kinafanya kazi kilikuwa ni
kiwanda tanzu cha kampuni ya Uingereza ya kusindika nyama ya Liebig’s
Extract of Meat Corporation (Lemco). Kabla ya kutaifishwa mwaka 1974,
TPL ilikuwa imeajiri watu 1,200.
Tanzania ilipata pigo kubwa wakati Lemco walipoondoa chata yao katika
leseni ya soko. Kuondolewa kwa leseni hiyo kulileta mgogoro mkubwa wa
uzalishaji na mwaka 1993 kiwanda kilifungwa rasmi. Wakati TPL ikifanya
kazi ilikuwa inachinja ng’ombe 550 kwa siku katika shifti mbili za
kufanyia kazi.
Kuanza kwa usindikaji huo katika kiwanda cha Nguru baada ya miaka 25
ya kuondoka katika soko la kimataifa kutasaidia ufugaji na wafugaji
ambao kwa sasa wanalalamikia soko.
Hii ina maana kwamba, wafugaji wa Tanzania sasa watakuwa na soko la
uhakika wa mifugo yao, kwani kwa kiasi hicho, ina maana kwa mwezi,
ng’ombe 9,000 watachinjwa, sawa na ng’ombe 108,000 kwa mwaka.
Aidha, mbuzi 60,000 watachinjwa kwa mwezi, sawa na mbuzi 720,000 kwa
mwaka. Aidha, kiwanda hicho ambacho kitapeleka asilimia 80 ya nyama
katika soko la nje, hasa nchi za Mashariki ya Kati na Mashariki ya
Mbali, kitatoa ajira za moja kwa moja kwa wafanyakazi 500 na nyingine
nyingi zisizo za moja kwa moja.
Mkurugenzi Mkuu LAPF, Elliud Sanga alisema hivi karibuni kuwa,
asilimia 20 ya bidhaa zinazozalishwa zitalenga soko la kimataifa,
asilimia 20 itakuwa kwa ajili ya hoteli za Tanzania, taasisi zenye
uhitaji wa nyama bora na ya uhakika, lakini pia kwa Watanzania kwa
ujumla, kwani itafikiria kuwa na maduka yake katika baadhi ya maeneo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu, LAPF imewekeza dola 3,900,000 (Sh
bilioni 8) na hivyo kumiliki asilimia 39 ya hisa zote, huku wawekezaji
wengine wakiwa kampuni ya Eclipse (asilimia 46) na Busara Investment
yenye asilimia 15. “Jamani, hii ni fursa ya kipekee kwa wakulima na
wafugaji wetu…
Ukiacha faida za moja kwa moja kwa moja kwa wafugaji na jamii
inayozunguka kiwanda, tutarajie pia ongezeko la fedha za kigeni kwa
kuuza bidhaa za nje na kuiinua sekta ya mifugo nchini,” alisema.
Aidha kuwapo kwa uzalishaji kutasaidia kuondokana na migogoro baina
ya wakulima na wafugaji katika maeneo mengi ya Tanzania kwa kuwa
wafugaji watakuwa na uhakika wa soko la mifugo.
Kuwapo kwa kiwanda hicho kumewezeshwa na Mfuko wa Pensheni wa LAPF,
ambayo imeungana na wadau wengine kuunga mkono kwa vitendo jitihada za
Serikali ya Awamu wa Tano ya Rais, Dk John Magufuli za kuifanya Tanzania
kuwa nchi ya viwanda na hivyo kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka
2015.
Naye mtaalamu katika sekta ya nyama, Cerusiri Badrinath, Ofisa
Mtendaji Mkuu wa Zubair Corporation ya Oman ambayo ni kampuni mama ya
Eclipse Investment yenye ubia katika kiwanda cha Nguru, alisema
wamechagua eneo sahihi la uwekezaji, kwani nchi za Mashariki ya Kati na
Mashariki ya mbali ni walaji wazuri wa nyama pengine kuliko sehemu
nyingine duniani.
“Mfano, wao wastani wa kula nyama ni kilo 66 kwa mtu, na kumbuka wapo
zaidi ya milioni 56… lakini kiwango cha dunia cha wastani wa kila mtu
kula nyama hakifikia hata kilo 50 kwa mwaka.
Inakadiriwa katika miaka mitatu ijayo kiwango kinaweza kufikia
asilimia 78. “Sasa hakika hili ni soko la uhakika mno. Kikubwa ni
kuhakikisha nyama inayotoka Tanzania inakuwa na ubora wa kimataifa, na
ndilo lengo letu. Hivi karibuni hawa waliagiza nyama yenye thamani ya
Dola za Marekani bilioni tano (Sh trilioni 12), hii si biashara ndogo
hata kidogo,” alifafanua.
Tanzania ndiyo ya kwanza kwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki (EAC)
kuwa na idadi kubwa ya mifugo. Kwa mujibu wa ripoti ya ufugaji ya
Wizara ya Mifugo ya mwaka 2013, Tanzania ina idadi ya ng’ombe zaidi ya
milioni 22.8, mbuzi milioni 15.5, kondoo milioni 6.9 na nguruwe milioni
2.1 milioni.
Aidha, kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), wakati Brazil
ikiongoza duniani kwa kuwa na ng’ombe milioni 211, Tanzania inashika
nafasi ya 11 duniani. Kwa Afrika, Tanzania ni ya tatu, ikitanguliwa na
Ethiopia yenye ng’ombe milioni 54 wanaifanya nchi hiyo ishike nafasi ya
tano duniani. Sudan yenye ng’ombe milioni 41.9 inashika nafasi ya pili
Afrika na ya saba duniani.
Kwa ukanda wa EAC, Tanzania inafuatiwa na Kenya yenye ng’ombe milioni
18.1, Uganda ng’ombe milioni 13, Sudan Kusini ng’ombe milioni 12,
Rwanda ng’ombe milioni 1.4 na Burundi ina ng’ombe 777,786.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari alipongeza
uwekezaji huo, akisema kwa yanayofanywa na wawekezaji kama LAFP yanatoa
taswira halisi kwamba, `Tanzania ya Viwanda Inawezekana’ na kwamba
unafungua fursa zaidi za ajira.
Regina Chonjo, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro anayekaimu pia Ukuu wa
wilaya ya Mvomero, alisema kuanzishwa kwa kiwanda hicho ni furaha kwa
wakulima na wafugaji ambao kwa miaka mingi walikuwa na migogoro kutokana
na wafugaji kudaiwa kuvamia maeneo ya wakulima na kulisha mifugo yao
mazao ya wakulima.
“Kwa ujio wa kiwanda hiki, nina uhakika ufugaji holela sasa utakoma
na watu watahamia kwenye ufugaji wenye tija. Kila mmoja atataka kufuga
kisasa ili kujiongezea kipato kwa sababu tayari kuna soko la uhakika, la
kila siku. Kuchinja ng’ombe 300 na mbuzi 2,000 kwa siku si mchezo.
“Lakini pia kuna manufaa mengi yatakayotokana na kiwanda hiki,
wakulima watauza majani kwa ajii ya mifugo, ajira zitaibuka, nyingi tu,
fursa mbalimbali zitaibuka kumbukeni kutakuwa na pia na pilika za magari
hapa… sasa ni wakati wa wenyeji wa Morogoro kujiandaa zaidi kwa fursa
zitakazofunguka hapa,” alisema.
Mbali ya nyama, ngozi na maziwa, kinyesi pia kitatumika kuboresha
kilimo cha majani na mazao mengine kuzunguka kiwanda, kutakuwa pia na
ufugaji wa kisasa wa samaki na kadhalika.
Kiwanda hicho kipo katika eneo lenye ukubwa wa ekari 6,000 ambapo
ekari 1,200 zimejengwa miundombinu ya malisho ya mifugo
itakayonenepeshwa katika kipindi cha siku 90 kabla ya kuchinjwa.
Tanzania ni nchi ya tatu barani Afrika kwa wingi wa mifugo ya asili,
lakini wafugaji wengi wamekuwa wakiishi maisha duni, kwani mchango wa
mifugo ni mdogo sana katika kubadili maisha ya wafugaji na kuchangia
ipasavyo katika pato la taifa.
Wakati katika nchi nyingine sekta ya mifugo ikitegemewa na kuwa
chachu ya kuinua uchumi wa wafugaji na taifa kwa ujumla, Tanzania
ilibaki nyuma, hivyo kuanzishwa kwa kiwanda cha Nguru sasa kitakuwa
kimeibua fursa mpya ya kuwaondoa wafugaji katika umasikini wa kipato.
KIWANDA KINGINE
Kuibuka kwa mradi wa kiwanda cha Nguru kumekuja wakati kiwanda
kingine, Meat King Limited kilichopo nje kidogo ya jiji la Arusha
kikitangaza kuwa mbioni kuanza kazi na kwamba kinatarajiwa kuzalisha
tani 900,000 za nyama kwa mwaka huku kikipanga kukidhi mahitaji ya soko
la ndani kabla ya kuingia katika soko la jumuiya ya Afrika mashariki
(EAC).
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Lesley De Kock,
watachakata mazao ya nyama na kufungasha, lakini pia watakuwa na duka la
jumla na rejareja. Awali, kiwanda hicho kilikuwa na uwezo wa kuzalisha
tani 300,000 za nyama kwa mwaka, lakini sasa wamejipanga kuzalisha tani
900,000 kwa mwaka.
UZALISHAJI NYAMA DUNIANI
Mwaka 2012, nyama ya takribani tani milioni 304 ilizalishwa duniani
na makadirio ya wastani wa matumizi ya nyama yalikuwa kilo 42.8 kwa kila
mmoja kwa mwaka kwa wakati huo. Mwaka 2014, FAO ilikadiria ongezeko la
uzalishaji wa nyama duniani kufikia jumla ya takribani tani milioni
311.6.
FAO inakadiria kwamba ifikapo Mwaka 2050 (Idadi ya watu Duniani
inakadiriwa kuwa bilioni 9.6), uzalishaji wa nyama duniani utafikia tani
milioni 455. Mpaka sasa, takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 2013 Brazil
iliongoza duniani kwa kuuza tani milioni 1.85 (asilimia 20.17 ya mauzo
duniani), ikifuatiwa na India tani milioni 1.77 (19.26%), Australia tani
milioni 1.59 (17.38%), Marekani tani milioni 1.17 (12.79%) na New
Zealand, tani 528,000 (5.77%) kwa Afrika, Afrika Kusini, yenye ng’ombe
milioni 14 tu, ndiyo inayoongoza, kwani iliuza nyama tani 13,000 na
inashika nafasi ya 22 duniani.
MAZIWA
Uzalishaji wa maziwa Duniani unakisiwa kuongezeka kwa zaidi ya
asilimia 50 kutoka tani milioni 482 Mwaka 1982 hadi kufikia tani milioni
754 Mwaka 2012. India inaongoza kwa uzalishaji maziwa duniani,
takribani tani 122 kwa mwaka, sawa na asilimia 16 ya maziwa yote ya
duniani. Inafuatiwa na Marekani, China, Pakistan na Brazil.
BIASHARA YA NGOZI
Ngozi za aina mbalimbali zinatokana na wanyama wanaochinjwa au
kuuawa. Kati ya Mwaka 2008 na 2013, FAO inakadiria uchinjaji kwa mwaka
ulikuwa hivi: kondoo 542.5 milioni na mbuzi milioni 426.6.
Afrika inakadiriwa kuwa na asilimia 15 ya jumla ya ng’ombe na
takribani asilimia 25 ya kondoo na mbuzi wote duniani. Hata hivyo, mbali
ya wingi huo wa mifugo, Afrika inazalisha asilimia 8 tu ya ngozi za
ng’ombe na takribani asilimia 14 tu ya ngozi za kondoo na mbuzi duniani.
Idadi ya ngozi zinazozalishwa kote duniani kwa mwaka inakadiriwa kuwa
takribani milioni 240. Matumizi ya kibiashara ya ngozi ni pamoja na
kutengeneza viatu, mabegi, nguo, mikanda, viti, sofa na kadhalika kwa
ajili ya soko la ndani na kwa masoko ya kimataifa.
Aidha, damu, mifupa na bidhaa nyingine zitokanazo na wanyama hao,
zinaweza kutumika kutengeneza chakula cha mifugo, hivyo kuongeza
mnyororo wa thamani wa kila kitokanacho na wanyama.
UFUGAJI WA KISASA
Kama ilivyo kwenye kilimo na uvuvi wa kisasa, hata ufugaji
unahitajika kuwa wa kisasa kwa lengo la kuwa na bidhaa bora sokoni. Na
ili kuufikia ubora huo, mambo kadhaa yanahitajika ambayo ni ardhi ya
malisho kwa wafugaji, matumizi makubwa ya sayansi, teknolojia na
ubunifu, rasilimali fedha, viwanda vya kuthaminisha na kukamilisha
utengenezaji wa mazao ya mifugo, lakini pia sera na sheria za kustawisha
ufugaji na wafugaji.
SEKTA YENYE NGUVU
Kwa mujibu wa Mwakilishi wa Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na
utafiti wa mifugo ya International Livestock Research Institute (ILRI)
Tanzania, Amos Omore, mifugo ni sekta yenye nguvu ya kuleta mabadiliko
kiuchumi.
Anasema mifugo ni rasilimali isiyoisha kwani ni jadidi na dunia
nzima, watu bilioni moja huishi kwa kutegemea mifugo hasa wanawake na
ajira kwa vijana. Asilimia 15 ya kalori na asilimia 25 ya protini
inatokana na wanyama ambao ni muhimu katika mlo kamili na kuongeza uwezo
kipato kwa idadi kubwa ya watu masikini.
Kwa mujibu wa Omore, ongezeko la thamani ya bidhaa za mifugo ni nzuri
hasa kwa kilimo biashara kutokana na kwamba bidhaa sita za kimataifa
zinatokana na kilimo ambacho chanzo chake ni wanyama ikiwemo (maziwa,
nyama ya nguruwe, nyama ng’ombe, kuku na samaki) ambayo thamani yake
inafikia Dola za Marekani bilioni 715.
Hilo si pato haba ukizingatia kuwa teknolojia inayotumika ni duni na
haina ubunifu wa kina. Hata hivyo, ingawa mifugo inachangia asilimia 40
ya Pato la Taifa katika nchi nyingi ambazo ni masikini zaidi duniani,
lakini zinapata asilimia 4 tu ya misaada ya maendeleo ya kilimo.
Kutokana na maelezo ya mwakilishi huyo, sekta ya mifugo Tanzania
huchangia wastani wa asilimia 13 ya Pato la Taifa ambacho ni kiwango cha
chini ikilinganishwa na nchi zenye mifugo wachache kama Botswana.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment