Home » » WALI BADO NJAA AFRIKA

WALI BADO NJAA AFRIKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

LICHA ya Tanzania kusifika kwa uzalishaji wa mpunga, uzalishaji huo bado hautoshelezi kusaidia nchi za Afrika ambazo hulazimika kutumika zaidi ya dola za Marekani bilioni tano (sawa na Sh. trilioni 11.2) kuagiza mchele toka nje ya bara hilo.
Kiasi hicho cha fedha, imeelezwa, hununua tani 14,000 milioni, sawa na asilimia 40 ya mahitaji.
Akizungumza katika warsha ya kilimo bora cha mpunga inayoendelea mjini Morogoro, kaimu mkurugenzi wa shirika la kimataifa la Africa Rice kwa nchi za kaskazini na kusini mwa Afrika, Josey Kamanda, alisema bado bara la Afrika linahitaji msukumo juu ya kuzalisha zao la mpunga.
Kamanda alisema bara hilo limekuwa na upungufu mkubwa wa mpunga kutokana na wakulima kutokuwa na nyenzo za kutosha kulima zao hilo hivyo maeneo mengi yanahitajika kuongezeka ili kuongeza uzalishaji wake.
“Mchele huo unaoingizwa kutoka mabara mengine ni kuonyesha namana gani bara la Afrika lisivyoweza kujitosheleza, kinachotakiwa sasa ni bara hili la Afrika kuongeza uzalishaji na kuacha kuagiza mchele huo na kuweza kujitegemea,” alisema Kamanda.
Aidha alisema jukumu la Africa Rice ni kuendelea kusaidia wakulima ili kukuza na kupata mazao mengi ya mpunga, na kuwafanya wakulima kuongeza kipato chao na uchumi wa nchi husika na hata kufikia mabara mengine duniani.
Akizungumza pia katika warsha hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunjo alisema wilaya yake imeendelea kuboresha na kusimamia mabonde na mito iliyopo ili uzalishaji wa mpunga uongezeke.
Aidha alisema elimu imetolewa ili isionekane kuwa zao hilo ni la chakula pekee na badala yake liwe la kibiashara zaidi na kuongeza mnyororo wa thamani kwa wakulima wake.
Alisema kuwa baada ya kuwaelimisha, wakulima sasa wameanza kupata mavuno mengi ambapo wanavuna kati ya gunia 45 hadi 50 kwa ekari tofauti na awali walipokuwa wakipata gunia 15 hadi 20.
Alizitaja baadhi ya changamoto zinazowapata wakulima na kushindwa kuzalisha kwa wingi kuwa ni pamoja upatikanaji wa pembejeo kwa gharama kubwa ukilinganisha na kipato cha mkulima.
Aidha, alisema kumekuwa na upatikanaji wa vifaa vya kulimia kuwa bei ya juu.

Chanzo:Nipashe

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa