Home » » SERIKALI YATUMIA BILIONI 85 KUPELEKA MAWASILIANO VIJIJINI

SERIKALI YATUMIA BILIONI 85 KUPELEKA MAWASILIANO VIJIJINI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akifafanua jambo katika kikao na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mjini Dodoma. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi Kakoso na kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Mawasiliano wa Wizara hiyo Eng. Angelina Madete. 
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Mawasiliano), Eng. Angelina Madete akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuhusu miradi ya maendeleo ya mawasiliano vijijini katika kikao kilichofanyika mjini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Kasoso, akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Kamati hiyo katika kikao kilichowakutanisha na uongozi wa Wizara ya  Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano  na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) mjini Dodoma. Kulia kwake ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Eng. Edwin Ngonyani.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga akiwaonesha wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu maeneo ya vijijini yaliyofikiwa na mawasiliano katika kikao na Kamati hiyo mjini Dodoma. Kulia ni Mhe. Dua Nkurua na kushoto ni Mhe. Rita Kabati wajumbe wa Kamati hiyo.

Serikali imesema kuwa imetumia shilingi Bilioni 85 kupeleka mawasiliano vijijini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kuzipatia ruzuku kampuni za simu za mkononi ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma za mawasiliano.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwenye Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu mjini Dodoma.

“Mfuko huu unaendelea kuhakikisha kuwa mawasiliano bora yanafika katika maeneo mengi nchini hususan vijijini na kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara ambapo Takwimu zinabainisha kuwa, tayari mawasiliano   yamefikishwa kwenye kata 443, vijiji 1,939  kuanzia mwezi Machi 2013 hadi Julai mwaka huu”, amefafanua Naibu Waziri Ngonyani.

Ameongeza kuwa tayari Mfuko umetiliana saini mkataba na kampuni za simu za mkononi mwezi Agosti mwaka huu kuhakikisha kuwa zinapeleka mawasiliano kwenye kata nyingine 75 na vijiji 154.

Aidha, ametanabaisha kuwa hadi hivi sasa asilimia 94 ya wananchi wanapata huduma ya mawasiliano nchini na kuongeza kuwa, Serikali kupitia mkataba wake na Kampuni ya Simu ya Halotel imefikisha mawasiliano kwenye jumla ya vijiji 3,069 kati ya vijiji 4,000 tangu walipoanza utekelezaji wa jukumu hilo mwezi Novemba, 2015 na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo ifikapo mwezi Novemba mwaka huu.


0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa