Na Jacquiline Mrisho
Kijiji cha Melela kilichopo wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro kimepitisha mpango wa matumizi ya Ardhi chini ya mradi
wa Ushiriki wa Wananchi katika Kusimamia Sekta ya Kilimo unaoratibiwa na Shirika lisilo la kiserikali la PELUM.
Kaimu
Mkurugenzi wa Wilaya ya Mvomero, Rugembe Maiga hivi karibuni alisema
kuwa mpango huo utasaidia kupunguza migogoro
ya ardhi wilayani Mvomero na kulishukuru shirika la PELUM kwa jitihada
zao za kupima vipande vya ardhi na kuwakabidhi hatimiliki makundi ya
wananchi yasiyojiweza.
“Sisi
kama Serikali tunalipongeza sana shirika hili hasa kwa kugusa kundi la
watu wasiojiweza ambalo linajumuisha wazee
kuanzia miaka 60, wajane, walemavu na watu wenye kipato kidogo kwenye
jamii lakini rai yetu kwenu ni kuwaomba kuendelea kutafuta miradi
mingine ambayo itahakikisha wanamfikia mwananchi mmoja mmoja wa kijiji
hiki ili kila mtu aweze kumiliki hatimiliki ya ardhi
yake na hata ikiwezekana kumalizia kupima vijiji 52 vilivyobaki katika
Wilaya yetu”, alieleza Maiga.
Maiga aliongeza kuwa kundi linalohudumiwa na PELUM Tanzania ni kundi sahihi kwani wengi wao ndio wamekuwa wakionewa
kwa kupokonywa ardhi zao na kuziuza hivyo hatua ya kuwapatia hatimiliki litasaidia kuondoa kero hizo.
Pia,
Kaimu Mkurugenzi huyo aliwakumbusha wanakijiji hao kuwa ni jukumu la
kila mmoja kusimamia na kutekeleza mpango
huo na hasa kwa kuzingatia njia za mifugo, maeneo ya malisho na sehemu
za kilimo kama wao wenyewe walivyoamua wakati wa kutambua, kupima na
kuandaa mpango huo wa matumizi ya ardhi ya kijiji cha Melela.
Kwa kuwa Kijiji hicho ni cha wakulima, Maiga alitoa rai kwa wanakijiji kutoa taarifa za wafugaji watakaovamia maeneo
hayo ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kabla hakujatokea madhara yoyote.
Aidha,
Maiga amesema kuwa Halmashauri ya Mvomero imejipanga kuhakikisha
inamalizia ujenzi wa masijala ya ardhi ya kijiji
hicho ili wananchi wapate eneo la kuhifadhi hati zao pia ameyashauri
mashirika mengine ya binafsi kuiga mfano wa shirika hilo kwani linalinda
maslahi ya ardhi kwa wananchi wote.
Kijiji
cha Melela ni moja kati ya Vijiji vitano vinavyofanyiwa Mpango wa
Matumizi ya Ardhi na Shirika la PELUM Tanzania,
jumla ya hatimiliki 500 toka vijiji vya Melela, Mlandizi, Magali,
Kibaoni na Mela vya Wilayani Mvomero zinatarajiwa kutolewa kwa makundi
ya watu wasiojiweza.
0 comments:
Post a Comment