WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mara ya kwanza
katika historia imelazimika kumteua Jaji kwa ajili ya kufanya uchunguzi
wa migogoro ya ardhi iliyoshindikana kupatiwa suluhu kwa njia ya
usuluhishi katika vijiji saba mkoani Morogoro.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Waziri wa wizara hiyo, William Lukuvi
alisema amemteua rasmi Jaji wa Mahakama Kuu, Kitengo cha Biashara,
Jacob Mwambegele kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi kufanya uchunguzi wa
migogoro hiyo kwa muda wa siku 60 akiwa na timu ya wataalamu wanane.
Alisema hatua hiyo ya kumteua Jaji kufanya uchunguzi kwa mujibu wa
sheria imefikiwa baada ya wizara hiyo kuchukua hatua zote za kutafuta
suluhu katika vijiji hivyo, vikiwemo viwili ambavyo migogoro yake
imekithiri ambavyo ni Kambala kilichopo wilayani Mvomero na Mabwegere
kilichopo wilayani Kilosa.
“Hii ni hatua yetu ya mwisho kama wizara katika kutafuta suluhu
kwenye vijiji hivi, hasa hivi vya Kambala na Mabwegere ambavyo
vilianzishwa rasmi mwaka 1989 vina migogoro mingi iliyosababisha maafa
kwa binadamu, wanyama na mimea. Hivyo tunahitaji tu kufuata sasa hatua
za kisheria,” alisisitiza Lukuvi.
Alisema kabla ya uteuzi wa Jaji Mwambegele, wizara hiyo ilishamteua
msuluhishi Stephen Mashishanga ambaye jitihada zake za kusuluhisha
migogoro hiyo zilishindikana na hata taarifa yake ya usuluhishi katika
vijiji hivyo ilikataliwa na wananchi.
Lukuvi alisema kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi endapo hatua zote za
kutafuta suluhu katika migogoro ya ardhi zitashindikana, hatua
inayofuata ni kumchagua mtu atakayefanya uchunguzi wa migogoro hiyo
mwenye uzoefu kisheria ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Chanzo Na Habari Leo
0 comments:
Post a Comment