Home » » PROF. MBARAWA AWAANGUKIA MAKANDARASI

PROF. MBARAWA AWAANGUKIA MAKANDARASI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewataka makandarasi waliosimamisha kazi, kuendelea na ujenzi baada ya serikali kuanza kuwalipa madai yao.
 
Profesa Mbarawa aliyasema hayo jana akiwa wilayani Mvomero,  Morogoro, baada ya kukagua ujenzi wa barabara ya Magole-Turiani yenye urefu wa kilomita 48.6.
 
Prof. Mbarawa alisema serikali imeshalipa makandarasi mbalimbali Sh. bilioni 400 na itaendelea kufanya hivyo ili kumaliza madeni yao kwa haraka.
 
 “Hakikisheni mnarejea kazini na kuwapa mikataba ya ajira wafanyakazi wenu katika kipindi cha wiki mbili kuanzia sasa ili ujenzi wa barabara na madaraja ukamilike kwa mujibu wa mkataba hivyo kuondoa usumbufu kwa watumiaji wa barabara hii,” alisema.
 
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa alikagua karakana ya ujenzi wa vichwa vya treni mjini Morogoro na kumtaka mkandarasi anayekarabati vichwa hivyo kufanya kazi hiyo kwa haraka na kutoa kazi zingine kwa Watanzania ili kuwajengea uwezo wa kazi hizo.
 
Aidha, Profesa Mbarawa aliwataka wafanyakazi wa Kampuni ya  Reli Tanzania (TRL), kufanya kazi kwa ubunifu, uadilifu na uwazi ili kufufua hadhi ya kampuni hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi wa nchi.
 
Alisema takribani asilimia 96 ya mizigo inayoshushwa katika Bandari ya Dar es salaam husafirishwa kwa njia ya barabara, hivyo ni jukumu la TRL kuhakikisha inapata mizigo ya kutosha ya kusafirisha.
 
Naye Mbunge wa Mvomero, Suleiman Sadik, aliiomba serikali kumalizia daraja la Diwale lenye urefu wa mita 75 ili liweze kupitika.
CHANZO: GAZETI LA  NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa