Home » » SERIKALI YAMTAKA KILA MWANAJAMII KUTAMBUA NA KUTHAMINI HAKI ZA WAZEE

SERIKALI YAMTAKA KILA MWANAJAMII KUTAMBUA NA KUTHAMINI HAKI ZA WAZEE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Na Magreth Kinabo –maelezo
30/09/2015
Serikali   imemtaka kila mwanajamii kutafakari haki ambazo wazee wanastahili na kuweka mipango ya makusudi katika kuwawezesha kuzipata haki hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,Dkt, Donan Mmbando kupitia tamko  la wizara hiyo kuhusu maadhimisho  ya siku ya kimataifa ya wazee duniani itakayofanyika kesho  Oktoba Mosi ,mwaka huu wilayani Kasulu mkoani  Morogoro.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Umuhimu  Kuwashirikisha Wazee Kwa Ustawi Endelevu Mijini”.

“Uko umuhimu kwa jamii yetu kutafakari iwapo tunatambua mahitaji halisi na kuthamini michango yao kama rasilimali muhimu katika maendeleo ya taifa.

“Tunawashirikisha, tunawaheshimu na kuwaendeleza kama wananchi wengine na tunaheshimu mila na desturi nzuri za kuwaenzi wazee hao,” alisema Dkt. Mmbando.

 Aliongeza kwamba wazee katika nchi yetu wanayo nafasi kubwa katika juhudi za kuleta maendeleo. Katika maisha ya kila siku ya jamii, wazee wanakubalika kuwa ni watoa habari, ujuzi wa mila na desturi, washauri na wapatanishi. Pia wazee ni walezi wa watoto wadogo,hususan kwa watoto yatima walioachwa na wazazi wao kutokana na janga la UKIMWI.

“ Natoa  wito kwa watendaji wote kwa nafasi zao mbalimbali hususan wakurugenzi watendaji  Halimashauri za Miji/Manispaa/Wilaya na wakala mbalimbali zinazotoa huduma kwa wazee ili ziweke mipango inayozingatia haki za wazee na kuimarisha mifumo ya kinga ya jamii iliyopo ili kuboresha huduma wanayopata,” alisisitiza.

Aidha Dkt. Mmbando alisema alisema suala la wazee ni mtambuka, hivyo kila idara na asasi mbalimbali za Serikali na watu binafsi zishiriki katika  kuhakikisha  kwamba  juhudi juhudi za makusudi zinafanywa ili kuboresha maisha ya wazee.

 Alisema Serikali itaendelea kutambua na kuthamini michango inayotolewa na  wazee katika maendeleo ya taifa letu.

“ Hivyo nawaomba wazee waendelee kushirikiana na Serikali yao katika kuendeleza utulivu  na amani tuliyonayo na pia waendelee kuwa kielelezo bora na urithi kwa vijana wetu kwa manufaa ya taifa letu,” alisema.

 Alitoa changamoto kwa vijana kuwa karibu na wazee ili kujifunza maadili mema toka kwao na kuwajibika kuwahudumia ipasavyo na kuweka taratibu za kujiwekea akiba kila wanavyopata ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kufanya maandalizi ya maisha kuelekea uzeeni.


0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa