Home » » Hili ni Tishio: 10 wadaiwa kukutwa na silaha, milipuko msikitini, Pia nguo za kijeshi, mmoja ajeruhi polisi kwa jambia

Hili ni Tishio: 10 wadaiwa kukutwa na silaha, milipuko msikitini, Pia nguo za kijeshi, mmoja ajeruhi polisi kwa jambia

 10 wadaiwa kukutwa na silaha, milipuko msikitini, Pia nguo za kijeshi, mmoja ajeruhi polisi kwa jambia, Wananchi wamuua kwa kumchoma moto.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani), milipuko inayodaiwa kuwa ni ya hatari ambayo iliyokamatwa juzi usiku kutoka kwa watuhumiwa tisa waliokuwa wamehifadhiwa ndani ya Msikiti wa Suni uliopo tarafa ya Kidatu wilayani Kilombero.PICHA: MPIGAPICHA WETU
Hofu ya kutokea kwa mashambulizi kwa kutumia milipuko imeibuka mkoani Morogoro, baada ya Jeshi la Polisi kudai kuwakamata watuhumiwa 10 wakiwa wamejificha msikitini wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi na vitu mbalimbali vya kufanyia uhalifu.
 
Aidha, mmoja wa watuhumiwa hao anadaiwa kuuawa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira, baada ya kumkata askari polisi shingoni kwa kutumia jambia.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paul, jana alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kwamba, tukio hilo lilitokea tarafa ya Kidatu, wilaya ya Kilombero.
 
Kamanda Paul alimtaja mtuhumiwa aliyeauwa kuwa ni Hamad Makwendo, mkazi wa Manyasini Ruaha, tarafa ya Kidatu, wilaya ni humo.
 
Alidai kuwa tukio hilo lilitokea Aprili 14, mwaka huu, saa 3:30 usiku, katika kitongoji cha Nyandero.
 
Kwa mujibu wa Kamanda Paul, mtuhumiwa aliyeuawa alikuwa kiongozi wa wenzake waliotiwa mbaroni na jeshi hilo.
 
Alisema siku ya tukio polisi walipata taarifa kwamba kuna watu wanajihusisha na uhalifu na kuanza kuwafuatilia kwa muda, lakini walikuta tayari wakiwa wameshaondoka kuelekea maeneo yasiyojulikana.
 
Kamanda Paul alidai polisi walipata taarifa kuwa watu hao walitumia usafiri wa bajaji.
 
Alisema wakati wakiendelea kuwafutilia, walikutana na bajaji moja ikiwa na abiria mmoja na kuisimamisha.
 
Kamanda Paul alisema bajaji hiyo iliposimama, Hamadi ambaye ni marehemu, aliruka na kuanza kukimbia.
 
Alidai askari mwenye namba F .3323 Koplo Nasoro alianza kumkimbiza na alipomkaribia, mtuhumiwa huyo alichomoa jambia na kumkata askari huyo shingoni ambaye alivuja damu nyingi.
 
Kamanda Paul alidai kuwa askari mwingine mwenye namba E9245 Koplo Chomola, aliyekuwa nyuma, alifanikiwa kumpiga mtuhumiwa risasi mguuni.
 
Alidai kuwa mtuhumiwa huyo alipoanguka chini, wananchi wenye hasira walifika eneo hilo na kuanza kumshambulia na kisha kumchoma moto.
 
Kutokana na hali hiyo, alidai kuwa walilazimika kuongeza kikosi cha askari kutoka mkoani ili kuendesha operesheni ya kuwasaka watuhumiwa wengine.
 
Kamanda Paul alidai kuwa wakiwa kwenye operesheni hiyo walipata taarifa kuwa baadhi ya watuhumiwa walikuwa katika msikiti wa Suni, uliopo eneo la Kidatu.
 
Alidai kuwa askari walifika katika msikiti huo na kuomba viongozi wake kwa kushirikiana na wa serikali kuwatoa watu wote waliokuwa msikitini ili kubaini watu wanaotiliwa shaka juu ya kuhusika na matukio ya kihalifu.
 
Kamanda alidai kuwa waumini wote walitakiwa kutoka nje ya msikiti wakiwa na mikoba yao.
 
Alisema baada ya hapo, polisi walianza kufanya ukaguzi na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 10 wakiwa na vifaa mbalimbali vya kufanyia uhalifu.
 
Kamanda Paul alidai vitu vilivyokutwa katika mikoba ya watuhumiwa hao ni pamoja na milipuko 30, bendera nyeusi yenye maandishi ya Mungu mmoja, nyaya za kulipulia milipuko (detonators), majambia, bisibisi, vifaa vya kuficha uso (masks), sare za jeshi, misumeno ya chuma, spana, madaftari na vitabu mbalimbali vikiwamo vya stakabadhi.
 
Alidai kuwa mbali na vitu hivyo, pia marehemu alikutwa na risasi sita, tano zikiwa za bunduki aina ya SMG na moja ya bunduki aina ya Mark IV pamoja na ‘detonators fuse’ mbili zikiwa katika mfuko mdogo wa jeshi.
 
Kamanda Paul alidai askari aliyejeruhiwa alipoteza damu nyingi na kwamba, alikimbizwa katika Hospitali ya Kiwanda cha Sukari cha Kilombero na hali yake inaendelea vizuri, huku taratibu za kumhamishia Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro zikiendelea kushughulikiwa.
 
NIPASHE jana iliwasiliana na imamu wa msikiti unaotajwa bila mafanikio.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa