Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani hapa,
kimetangaza kuanza kutoa fomu leo kwa wanachama wanaotaka kuwania
nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi ya wilaya na jimbo huku
kikitahadharisha vitendo vya rushwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Chama cha
Waandishi wa Habari mkoani hapa (MOROPC), Katibu wa CHADEMA Mkoa wa
Morogoro, Ngonyani Ngonyani, alizitaja nafasi zinazowaniwa kuwa ni
mwenyekiti, katibu, katibu mwenezi, mweka hazina, wajumbe wa kamati
tendaji na mabaraza yote ya chama ikiwemo vijana, wanawake na wazee.
Alisema fomu hizo zinatolewa kwa gharama ya sh 10,000 kwenye ofisi
zote za kata, wilaya na kwenye tovuti ya chama na zinatakiwa kuwa
zimerudishwa Agosti 7 saa 10 jioni kisha mchujo utafuata Agosti 8 na 9.
Kwa mujibu wa katibu huyo, mkoa una wilaya saba na majimbo 10, na
kwamba tofauti na chaguzi zilizopita, sasa hivi makatibu watajaza fomu
kama nafasi nyingine na zitapelekwa taifani kupitiwa na kuteuliwa na
kamati kuu ya uteuzi.
“Uchaguzi wetu ni tofauti na vyama vingine, maana hatuna kampeni,
mpaka sasa tayari tunashirikiana na makachero wetu na Takukuru
kudhibiti udanganyifu, lakini kama haitoshi baada ya mchujo Agosti 9,
Agosti 10 tunakutana ukumbini na kila mtu atajinadi na kuchaguliwa moja
kwa moja,” alifafanua.
Alisema wote watakaokamatwa kwa rushwa au kuwa na harufu ya rushwa,
majina yao yataondolewa moja kwa moja kwenye kinyang’anyiro na
kuburuzwa kwenye nyombo vyenye mamlaka vikiwemo vya sheria.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment