Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wafanyabiashara wadogo na wa kati wamekuwa katika wakati mgumu
wa kupanua biashara zao kutokana na taasisi za fedha kutoa mitaji ya
muda mfupi kwa ajili ya kuendesha biashara badala ya kutoa mitaji ya
muda mrefu yenye masharti nafuu.
Utaratibu huo wa taasisi za fedha umesababisha
biashara kukua polepole na kukwamisha fursa nyingi za kibiashara, licha
ya wafanyabiashara wadogo na wa kati kutoa mchango mkubwa katika uchumi
wa taifa.
Kutokana na kuwapo kwa changamoto hiyo, mwaka huu
waandaji wa bajeti wameshauriwa kuifanyia kazi Sera ya Uchumi na
Uwezeshaji ya Taifa ya mwaka 2004 kwa lengo la kuiwezesha sekta binafsi
kujiendesha katika mazingira mazuri.
Lakini siyo hayo tu, bali licha ya kuwapo kwa
mifuko ya fedha za uwezeshaji kwa mfano, mfuko wa uwezeshaji wa
mwananchi na mfuko wa uwezeshaji wa uchumi na mpango wa ajira (J.K.
Fund), upatikanaji wa mitaji umekuwa ni tatizo kwa wafanyabiashara
kutokana na kutokuwapo kwa mazingira rafiki kwenye taasisi za fedha.
Kwa mtazamo wa jicho la pili, Tanzania imejitahidi
kuanzisha taasisi za kukopesha wafanyabiashara kwa mfano, Benki ya
Maendeleo Tanzania (TIB), lakini imeshindwa kuzipatia fedha za kutosha
kwa ajili ya kutoa mikopo ya muda mrefu kwa wafanyabiashara.
Kwa mujibu wa utafiti kuhusu wafanyabiashara
wadogo na wa kati, uliofanywa na Atsede Woldie, John Isaac Mwita na
Joyce Saidimu, taasisi za fedha zimeshindwa kuwawezesha wafanyabiashara
hao kutokana kukosa maarifa ya kuendesha miradi ya kibenki na kuwapo kwa
gharama kubwa katika utoaji wa huduma za kifedha.
Kutokana na mazingira hayo, sekta binafsi
imeishauri Serikali kuweka mazingira mazuri ya kupatikana kwa mitaji ya
kutosha katika bajeti ijayo.
Mbali na hoja hizo, wafanyabishara hao kwa nyakati
tofauti wanasema kuwa mazingira magumu ya upatikanaji wa mikopo kutoka
taasisi za fedha, ni kikwazo cha kutokua kwa biashara zao.
Mhadhiri wa uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Profesa Humphrey Moshi anasema serikali inapaswa kuzishawishi
benki ili zitoe huduma maalumu za kifedha kwa wafanyabiashara.
Profesa Moshi anasema benki hizo zinapaswa kutoa
mikopo ya muda mrefu yenye masharti nafuu kwa wafanyabiashara kwa lengo
la kukuza biashara zao.
“Kwa mfano, benki zote za India, zina madirisha
maalumu kwa ajili ya kusaidia shughuli za kilimo na madirisha mengine
maalumu yanayotoa huduma za kifedha kwa wafanyabiashara wadogo na wa
kati. Mkakati huo unapaswa ufanyike hapa kwetu. Naamini kama serikali
itafanya hivyo uchumi wa taifa utakua vizuri.
“Sekta isiyo rasmi nchini ina wafanyabiashara
wadogo milioni 3 ambao wanachangia asilimia 48 ya uzalishaji wa ndani na
kutengeneza ajira nchini kwa asilimia 26.
“Wafanyabishara wa wadogo na kati ni kundi muhimu katika ukuaji
wa uchumi katika mataifa duniani pia wanatengeneza ajira mbalimbali.
Serikali inapaswa kuwasaidia wafanyabiashara ili wapate mikopo yenye
masharti nafuu na kuinua biashara zao,” anasema Profesa Moshi.
Profesa Moshi anaishauri Benki Kuu ya Tanzania
(BoT) kuzifuatilia taasisi za fedha ili zipunguze riba katika mikopo
inayotoa kwa wafanyabiashara.
“Kumekuwapo kwa ongezeko kubwa la taasisi za fedha
kama vile, Ushirika wa Kuweka na Kukopa (Saccos) na Vikoba ambazo
hazifuatiliwe BoT. Taasisi hizi zinatoa mikopo kwa riba kubwa na wakati
mwingine wanachangia kufa kwa biashara kutokana na wakopaji kushindwa
kurejesha mikopo,” anaeleza Profesa huyo.
Mkurugenzi mtendaji wa mfuko wa sekta binafsi,
Godfrey Simbeye anasema katika bajeti ijayo, Serikali inapaswa kutenga
fedha kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wajasiriamali kama inavyofanya
katika sekta nyingine nchini.
“Elimu kwa wajasiriamali ni muhimu kwa kuwa wengi wanashindwa kufanya biashara kitaalamu,” anaeleza Simbeye.
Simbeye anasema Serikali inapaswa kuboresha Wizara
ya Viwanda na Biashara na kuongeza fedha zaidi TIB kwa lengo la
kuiwezesha kutoa mikopo ya muda mrefu kwa wafanyabiashara.
Kwa mujibu wa Simbeye, mitaji imekuwa ni tatizo
kwa wafanyabiashara kwa kuwa wengi wao wameshindwa kufanya biashara na
wenzao wa nje ya nchi.
“Kuwekeza katika miradi mikubwa, unapaswa kuwa na
fedha nyingi na hii inawezekana, endapo taasisi za fedha zitakuwa
zikitoa fedha za kutosha, lakini hilo Tanzania halifanyiki.
“Serikali ina wajibu wa kutuwezesha kupitia benki
yake ya TIB, ili iwe rahisi kwa sekta binafsi kukopa fedha nyingi kwa
ajili ya miradi mbalimbali.
“Katika mwaka huu wa fedha, sijui Serikali
imetenga shilingi ngapi katika Benki ya TIB, lakini naamini kwamba kiasi
cha fedha kilichotengwa hakitatosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo,”
anabainisha Simbeye.
Katika hatua nyingine, Simbeye anasema katika
mpango wa maendeleo wa mwaka 2011/12 hadi 2015/16, sekta binafsi
inatakiwa kuchangia Dola 6 bilioni za Kimarekani kila mwaka ikiwa ni
kutekeleza mpango huo.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment