Home » » MVUA ZAUA WATOTO ,BARABARA ZAFUNGWA MORO

MVUA ZAUA WATOTO ,BARABARA ZAFUNGWA MORO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam  wakichimba udongo chini ya Daraja la Mto Msimbazi lililopo Tabata Matumbi jana kutafuta miili ya ndugu zao waliozolewa na mafuriko kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Watoto watano wamekufa maji katika maeneo mbalimbali mkoani Morogoro na mwingine Dar es Salaam jana baada ya kutumbukia kwenye mito na mashimo yaliyofurika maji ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.
Vifo hivyo vinafanya idadi ya watu walipoteza maisha tangu mvua hizo kubwa zilipoanza Aprili 10, mwaka huu kufikia takriban 16 na kusababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara, makazi ya watu na mazao.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Elias Tarimo alisema jana kwamba mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kilosa, anahofiwa kufa maji baada ya kuzama katika Mto Ludewa alipojaribu kuvuka akitokea shuleni.
Tarimo alisema hadi kufikia jana asubuhi, mwili wa mwanafunzi huyo ambaye jina lake halijafahamika, ulikuwa bado haujapatikana.
Habari kutoka Kilombero zinasema watoto wawili wa familia moja katika Kitongoji cha Godauni, Kijiji cha Mkangawalo, Tarafa ya Mngeta, wamekufa maji baada ya  kutumbukia kwenye shimo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile aliwataja watoto hao kuwa ni Festo Andrew (3) na Chrisantus Mnanagali (11) na kwamba walitumbukia shimoni baada ya kuteleza walipokuwa wakicheza.
Shilogile alisema katika tukio jingine, watoto wengine wawili wa familia moja, nao walikufa maji baada ya kuzama walipokuwa wakivuka Mto Morogoro katika eneo la Mlimani.
Hata hivyo, alisema wazazi na ndugu wa watoto hao waligoma kutoa taarifa polisi na badala yake walichukua miili ya marehemu iliyokuwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Morogoro.
Taarifa zilizotolewa na Wakuu wa Wilaya za Kilombero, Kilosa, Ulanga na Mvomero, mvua hizo zimeathiri kwa kiasi kikubwa mashamba, miundombinu ya barabara, majengo ya umma na makazi ya wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Hassan Masala alisema Barabara za Mlimba- Ifakara na Chita-Mbingu, zimefungwa na huduma za usafiri zimesitishwa kutokana na uharibifu huo.
Alisema tayari ameshatoa taarifa kwa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), ili kufanya tathmini ya uharibifu wa barabara hizo na kufanya matengenezo ya haraka ili kurudisha huduma za usafiri.
Mkuu wa Wilaya ya Ulanga, Francis Miti alisema mvua hizo zimesababisha uharibifu mkubwa katika Tarafa ya Malinyi ambako baadhi ya barabara hazipitiki.
Alisema nyumba na mashamba mengi vimeharibiwa na mvua hizo na tayari amewatuma maofisa wake kufanya tathimini ya uharibifu huo.
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka alisema Barabara ya Mgeta-Nyandira imesombwa na maji hivyo kukwamisha huduma za mawasiliano na uchukuzi. Barabara hiyo kwa sasa imefungwa kwa muda hadi hapo itakapofanyiwa matengenezo.
Katika Manispaa ya Morogoro, barabara zilizoharibiwa na mvua ni Barabara Kuu ya Morogoro - Dodoma eneo la Kihonda Mbuyuni jirani na Mto Ngerengere ambako imeanza kutitia. Tanroads imeifunga upande mmoja ili kuepusha maafa hali ambayo imesababisha foleni na usumbufu kwa abiria na watumiaji wengine.
Mmoja afariki Dar
Taarifa za Polisi Mkoa wa Ilala zimesema mtu mmoja aliyetambulika kwa jina moja Mkojani (30) alifariki dunia juzi saa 11 jioni maeneo ya Segerea kwa Bibi alipokuwa akivuka maji.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema mtu huyo alikuwa akiendesha bodaboda na alikufa baada ya kupita kwenye maji hayo na kuingia katika dimbwi lililokuwa na nyaya za umeme na kusababisha kifo chake.
Alisema watu walioshuhudia tukio hilo walisema mtu huyo alikaidi wito wa kutopita hapo kutokana na kuanguka kwa nyaya hizo. Katika tukio jingine alisema mkondo wa maji unaounganisha Chanika na Nyeburu umefurika na kusababisha eneo la Barabara ya Chanika kukatika.
Kwa upande wake, Kamanda wa Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo alisema Daraja la Mto Kizinga lililopo Kongowe ambalo linaunganisha Kigamboni na Mbagala limepata ufa na halifai kutumika.
“Hali ni mbaya sana ninavyokueleza nipo hapa na nimeshindwa kupitisha gari langu. Tunawaomba wananchi wasipitishe magari yao eneo hili kwa kuwa muda wowote linaweza likakatika,” alisema Kiondo.
Arusha yachukua tahadhari
Mkoa wa Arusha umeanza kuchukua tahadhari ya kukabiliana na madhara ya mafuriko kwa kuviweka tayari vikosi na kukusanya vifaa vya uokoaji.
Pamoja na vikosi na vifaa vya uokoaji, uongozi wa mkoa pia umeanza kukusanya bidhaa mbalimbali kama magodoro, mashuka, mablanketi na vyakula kwa ajili ya waathirika iwapo eneo lolote ndani ya mkoa litakumbwa na mafuriko.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo alisema  licha ya tukio la kukatika kwa daraja linalounganisha Wilaya za Monduli na Karatu eneo la Mto wa Mbu, hakuna jingine la mafuriko lililotokea mkoani mwaka huu hadi kufikia jana mchana.
Chanzo;mwananchi

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa