
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu
(wa pili kulia) akisisitiza jambo wakati wa ziara yake katika shamba la
Mkulazi lililopo katika kata ya Mkulazi mkoani Morogoro Alhamis wiki
hii. Wengine ni Meneja Kitengo cha Ardhi kutoka Kituo cha Uwekezaji
Nchini (TIC), Bw. Desiderius Narwango (kushoto) Mkurugenzi wa Huduma wa
TIC, Bi. Nakuala Senzia (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro vijijini,
Bw. Said Amanzi (wa pili kushoto).

Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu
(wa pili kulia) akimsikiliza Meneja Kitengo cha Ardhi kutoka Kituo cha
Uwekezaji Nchini (TIC), Bw. Desiderius Narwango (kushoto) wakati wa
ziara katika shamba la Mkulazi lililopo katika kata ya Mkulazi mkoani
Morogoro Alhamis wiki hii. Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma wa TIC, Bi.
Nakuala Senzia na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro vijijini, Bw. Said Amanzi
(wa pili kushoto).
Na Mwandishi wetu, Morogoro.
Serikali
imewakikishia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwa itaendelea
kuhakikisha kuwa inajenga miundombinu imara na muhimu kama barabara ili
kufanya kazi zao kuwa nyepesi na hivyo kufikia maendeleo.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, Dkt. Mary Nagu
alitoa kauli hiyo katika eneo la kata ya Mkulazi, Wilaya ya Morogoro
vijijini Mkoani humo Alhamis wiki hii, wakati alipofanya ziara katika
shamba la Mkulazi linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa hekta 63 elfu.
Alisema
siku zote wawekezaji wanapenda maeneo ambayo yanafikika kwa wepesi ili
waweze kufanya biashara kwa uhuru, hivyo ni wajibu wa serikali
kuiimarisha na kujenga mipya zaidi ili kuweka mazingira bora ya biashara
nchini.
Alisema
shamba la Mkulazi ni kubwa na wawekezaji wapo tayari kuwekeza hasa
katika kilimo cha miwa hivyo ni jukumu la kituo cha uwekezaji nchini
kuiona changamoto hiyo ili waweze kuwasiliana na mamlaka husika katika
kuboresha miundombinu ya barabara.
“Hii
ni changamoto kubwa, naomba tushirikiane wote kwa pamoja ili tuweze
kulifanyia kazi jambo hili kwa haraka na mafanikio,” alisema waziri
huyo.
Alisisitiza
kuwa nchi itaondokana na umasikini kwa kiasi kikubwa iwapo dhamira
itaelekezwa kwenye uwekezaji wa kilimo hasa katika mashamba makubwa ya
mazao mbalimbali kama sukari na mpunga.
“Hivi
sasa nchi yetu inaupungufu wa sukari hivyo uwepo wa wawekezaji katika
sekta hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hili,”
alisisitiza Dk. Nagu.
Aliongeza
kuwa serikali itaendelea kutenga maeneo mengi kwa ajili ya uwekezaji na
kuisisitiza kuendelea kutangaza vivutio vilivyopo katika nchi ili
wawekezaji wengi waweze kuja na kuwekeza na hivyo kuinua uchumi wa nchi.
“Kwa kufanya hivyo tutapiga hatua kubwa katika uwekezaji,” aliongeza.
Awali
akitoa maelezo kuhusu shamba hilo la Mkulazi, Mkurugenzi wa Huduma
kutoka Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), Bi Nakuala Senzia, alisema
tayari wataalamu wameshafika na kupima shamba hilo na tayari
limegawanywa kulingana na matumizi.
“Shamba
hili tayari limekwishagawanywa kulingana na matumizi ya wale
watakaohitaji kuwekeza, vibali vimekwishatolewa tunachosubiri ni mkataba
kutoka wizara ya ardhi,” alisema Mkurugenzi huyo.
Aliongeza
kuwa kwa sasa wameshafanya mawasiliano na kambi ya jeshi ya Ngerengere
ili waweze kusaidia kusafisha eneo la shamba hilo liwe katika muonekano
mzuri tofauti na ule wa sasa.
“Tayari
tumekwishaomba msaada wa jeshi la wananchi Ngerengere ili waweze
kutusaidia na wako tayari kwa msaada huo, hivyo baada ya siku kadhaa
muonekano washamba hili utakuwa katika hali nzuri,” alisisitiza.
Eneo
la Mkulazi lililopo katika wilaya ya Morogoro vijijini ni eneo
linalopitiwa na mito ya Ngerengere na Ruvu, na tayari baadhi ya
wawekezaji walishafika na kujionea eneo hilo ambalo mazao kama miwa na
mpunga yanatajwa kuwa yanaweza kustawi kwa wingi.
0 comments:
Post a Comment