Home » » PINDA;SIPATI USINGIZI

PINDA;SIPATI USINGIZI

image

WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amesema mafuriko yaliyotokea Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro, yanamfanya akose usingizi hasa baada ya kukatika Daraja Mkundi ambalo linaunganisha Barabara Kuu ya Morogoro-Dodoma hivyo kusababisha maji mengi kuingia vijijini.
Bw. Pinda aliyasema hayo Dar es Salaam jana baada ya kufanya ziara wilayani humo ili kujionea madhara yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo.
Alisema Serikali imeanza kufanya mikakati ya haraka ili kuhakikisha huduma za kijamii na kiuchumi zinarudi kama ilivyokuwa awali katika vijiji vilivyoathirika.
"Haya mafuriko yametokea juzi alfajiri na kusababisha maji mengi kutokana na mvua zilizonyesha Mikoa ya Manyara na Arusha, hivyo kusababisha wakazi wa kata za Magole, Belege, Msowelo kuathirika," alisema.
Aliongeza kuwa, Shule ya Sekondari ya Dakawa, Chuo cha
Ufundi VETA na Chuo cha Ualimu navyo vimeathiriwa lakini daraja la Mkundi ndilo linalomnyima usingizi zaidi baada ya kukatika mita 20 upande mmoja na 40 upande mwingine.
Bw. Pinda alisema, Mkuu wa Mkoa huo Bw. Joel Bendera amelazimika kubomoa tuta ili kuruhusu maji kutawanyika ambayo yangeathiri zaidi wananchi kwa upande mmoja
"Hadi sasa, haya mafuriko yamesababisha kifo cha mtu mmoja, kuharibu nyumba nyingi na kusababisha hasara kubwa ya mali, mifugo pamoja na mazao.
"Tayari Serikali imechukua hatua za haraka pamoja na kumuomba Mkandarasi anayejenga Barabara ya Kilosa kujaza mawe lori 50 katika upande wa kutokea Morogoro- Dumila na lori 50 za mawe kwa upande wa Dodoma ili kuyazuia maji," alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Magufuli amelazimika kuweka kambi eneo hilo ili ukarabati na ujenzi wa barabara hiyo uweze kufanyika haraka na kuruhusu magari kupita kuanzia leo.
Hadi sasa, msaada wa fedha sh. milioni 50 zimetolewa na Serikali, wahisani pamoja na vitu mbalimbali kama blanketi, vyakula, dawa, sabuni, mikeka, mahema na vyandarua.
Ka t ika ha tua ny ing ine , Waandishi Wetu Severin Blasio na Lilian Justice, kutoka Morogoro wanaripoti kuwa, zaidi ya kaya 500 katika Kijiji cha Magole, wilayani humo hazina makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji.
Mvua hizo pia zilisababisha madhara kwa mifugo ambayo ilisombwa na maji, kufa na kuharibu mazao mbalimbali.
Wakizungumza na Majira jana, wakazi wa kijiji hicho walisema mvua hizo zimewatia umaskini na hakuna misaada yoyote ya kibinadamu waliyoipata kutoka serikalini.
Bw. Juma Khamis na Mwanaidi Athuman, walisema hawajui hatima ya maisha yao hivyo wameiomba Serikali iwapelekee misaada ya haraka ili kunusuru maisha yao.
Wakati huo huo, zaidi ya watu 7,000 waliopo katika kata tatu zilizopo Tarafa ya Magole, wilayani humo hawana makazi ya kuishi baada ya nyumba zao kusombwa na maji.
Katika Vijiji vya Mbigili na Magole, karibu wakazi wake wote hawana makazi kutokana na nyumba zao ambazo ni za udongo kujaa maji yaliyofurika katika Mto Mkundi.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Elias Tarimo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa wilayani humo, amekiri mvua hizo kuleta madhara makubwa kwa wananchi.

Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa