Home » » Prof. Muhongo amuwakia mkandarasi wa umeme

Prof. Muhongo amuwakia mkandarasi wa umeme

Waziri wa Nishati na Madini,Profesa Sospeter Muhongo
 
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, `amemuwakia' mkandarasi wa  kusambaza umeme vijijini kutokana na kutokamilisha na kuzorota kwa miradi hiyo.
Mkandarasi huyo ni Meneja Mwendeshaji wa Miradi ya Umeme  Vijijini (Rea), MCC na Symbion, John Brady.

Kutokana na hali hiyo, Profesa Muhongo amemwagiza mkandarasi huyo kukamilisha miradi yote ifikapo Desemba 31, mwaka huu vinginevyo serikali itamchukulia hatua kali.

Alitoa agizo hilo baada ya kusomewa  taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo kutoka kwa Meneja wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Deogratias Ndamugoba.

Katika taarifa hiyo, Ndamugoba alisema mpaka sasa utekelezaji wa miradi hiyo umefikia asilimia 40 tu.

Waziri  Muhongo alianza juzi ziara ya siku tatu mkoani Morogoro kwa kukagua miradi ya usambazaji umeme vijijini iliyopo kwenye  Wilaya za Morogoro, Mvomero na Kilosa.

“Kwanini mpaka sasa ifikie asilimia 40? Hicho ni kiwango kidogo sana na hakuna sababu ya miradi kushindwa kukamilishwa kwa wakati. Hivyo kwa mradi wa MCC ninampa mkandarasi huyu hadi Novemba 30, mwaka huu awe amekamilisha na miradi yote ya Rea, awe amekamilisha ifikapo Desemba 31, mwaka huu vinginevyo tunaweza kuchukua hatua kama serikali,” alisisitiza Profesa Muhongo huku akionekana dhahiri kuchukizwa na hali hiyo.

Utekelezaji wa miradi mingi ya MCC na Rea ulianza kati ya mwaka 2011 na 2012 ambapo baadhi ilitakiwa ikamilishwe Agosti na Desemba, mwaka huu.

Akizungumza na wananchi wa vijiji vya Mtombozi, Mtamba na Ng’ongolo, Profesa Muhongo alisema serikali imedhamiria kuwaondolea wananchi umaskini kwa kuwawekea umeme ili waongeze vipato vyao kupitia sekta za kilimo na biashara.

Awali, Meneja wa Tanesco Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Ndamugoba, alisema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa miradi yote ya MCC, ina thamani ya Dola 17,930,644.05 za Marekani.

Hata hivyo, Meneja Mwendeshaji wa miradi ya Rea, MCC na Symbion, Brady, alimhakikishia Waziri Muhongo kuwa miradi yote hiyo itakamilika kwa muda aliopewa.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa