Home » » MNEC akemea vijembe, majungu

MNEC akemea vijembe, majungu

Morogoro. Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM, Suleiman Sadiq amewataka viongozi mbalimbali nchini kuhakikisha wanasimamia vyema miradi inayoanzisha na Serikali ili kutekeleza ilani ya chama hicho.
Akikagua uhai wa chama na miradi ya maendeleo katika Kijji cha Manyinga, Kata ya Diongoya, wilayani Mvomero, Sadiq alisema ni wajibu wa kila kiongozi aliyechaguliwa na CCM kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kikamilifu na kuachana na vijembe au majungu.
Sadiq alisema kufanya hivyo ni kurudisha nyuma jitihada za Serikali kuwaletea wananchi wake maendeleo.
‘’Tunataka kuhakikisha kila kiongozi anawajibika kwa nafasi yake kuleta maendeleo eneo lake kwa kutekeleza ilani ya chama, siyo kutupiana lawama mtu anapokosea ni vyema akashauriwa na kurekebishwa,” alisema Sadiq.
Pia, alisema iwapo viongozi waliochaguliwa au mwanaCCM yeyote atakwenda kinyume na chama, itasababisha chama kudhofika na kupoteza majimbo kwa wapinzani.
Sadiq alisema hawawezi kukubali hali hiyo itokee kwa sababu CCM ni imara na sikivu kwa wananchi wake, hivyo haina budi kukilinda kwa gharama yoyote ile.
Pia aliwataka viongozi wa mashina na matawi kuhamashisha wananchi kulipia ada zao za uanachama ili wawe hai sambamba na kuchangia shughuli au miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayoanzishwa katika maeneo yao ili kuharakisha maendeleo kwani serikali pekee haiwezi kutekeleza yote.

Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by : Tone Media
Copyright © 2012. Morogoro Yetu - All Rights Reserved
Template Modify by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa