BARAZA la Katiba lililoandaliwa na asasi zisizo za
kiserikali mkoani Morogoro za Volunteer Group na Kijogoo Group, limeitaka Tume
ya Mabadiliko ya Katiba kuondoa neno Tanzania Bara katika rasimu iliyopo na
kurejesha Tanganyika ili kukamilisha Muungano.
Baraza hilo lilitoa pendekezo hilo hivi katika
mkutano uliofadhiliwa na Foundation For Civil Society mjini hapa.
Pendekezo hilo lilikwenda sambamba na kuunga mkono
muundo wa serikali tatu kwenye rasimu hiyo na kutaka kuongezwa neno ‘usawa’
kwenye mambo ya Muungano kama dira ya mshikamano baina ya Zanzibar na
Tanganyika.
Baadhi ya washiriki wa baraza hilo lililokuwa na
washiriki zaidi ya 200; Ramadhan Chakachale na Upendo Rajabu kwa nyakati
tofauti walisema kimsingi rasimu imeandaliwa vizuri licha ya marekebisho madogo
kama yanavyojitokeza.
“Kimsingi sisi tumechelewa sana, ilitakiwa serikali
yetu ya Tanganyika tuidai tangu mwaka 1964, kwani wenzetu licha ya kuungana
bado waliendelea kuwa na serikali,” alisema Upendo.
Aidha, kutokana na kuanza kushamiri kwa dawa za
kulevya, Katiba itamke kuwanyonga watakaobainika sambamba na watakaokumbwa na
makosa ya mauaji na ufisadi.
Waratibu wa baraza hilo akiwamo Mwenyekiti wa
Volunteer Group, Avelyni Ligohalimu na Ramadhan Said wa Kijogoo Group, walitaka
washiriki kutafakari kwa kina marekebisho katika rasimu hiyo na kuchangia kwa
kina, ili mawazo yao yapenye na kuingia kwenye Katiba.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment